Kufanya jimaa mara nyingi bila kutawadha baina yake

Swali: Je, inafaa kwa mume kumjamii mke wake mara mbili pasi na kuoga kati ya mfano wa randi ya kwanza, ya pili na ya tatu?

Jibu: Inafaa kwake kufanya hivo licha ya kwamba bora ni kuoga. Imepokelewa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yanayojulisha juu ya kufanywa na kuachwa kwake. Watunzi wa as-Sunan na Ahmad wamepokea kupitia kwa Raafiy´ bin Khadiyj kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) usiku mmoja aliwazungukia wakeze ambapo anaoga kwa huyu na huyu. Kukasemwa: “Ee Mtume wa Allaah! Kwa nini usifanye josho moja?” Akasema:

“Hivi ndivo takasifu na vizuri zaidi.”

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwazungukia wakeze kwa josho moja.

Sunnah ni kwamba anapotaka kurudia kufanya tendo la ndoa bila kuoga basi angalau atawadhe wudhuu´ kama wa swalah. Pia kumepokelewa yanayojulisha juu ya kuacha kutawadha. Yanayofahamisha juu ya usuniwaji wake ni yale aliyopokea Muslim na wengineo kupitia kwa Abu Sa´iyd (Radhiya Allaahu ´anh) aliyeeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atapomwendea mmoja wenu mke wake kisha akataka kurudia, basi atawadhe.”

Imekuja katika upokezi wa Ibn Khuzaymah:

“Atapomwendea mmoja wenu mke wake kisha akataka kurudia, basi atawadhe wudhuu´ wa swalah.”

Kuhusu yanayojulisha kuacha ni yale aliyopokea at-Twahaawiy kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akijamii kisha anarudia na wala hatawadhi.”

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/187)
  • Imechapishwa: 29/08/2021