Du´aa za pamoja kila baada ya Rak´ah mbili za Tarawiyh

Swali: Katika kijiji chetu watu wanasoma katika swalah ya kisimamo cha usiku katika Ramadhaan Suurah “al-Ikhlaasw”, pamoja na “Subhaan Allaah”, “Alhamdulillaah”, “Allaahu Akbar” na “Laa hawlah wa laa quwwatah illaa billaah al-´Adhwiym” kwa pamoja kila baada ya Rak´ah mbili kwa kunyanyua sauti, jambo ambalo linaondosha utulivu. Je, kusema hivi Sunnah yoyote takasifu?

Jibu: Kitendo hichi ni Bid´ah na haifai kukifanya. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote mwenye kuzua katika dini yetu hii kisichokuwemo basi atarudishiwa mwenyewe.”[1]

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

“Yeyote atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”[2]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema katika Khutbah ya ijumaa:

“Amma bad´; hakika mazungumzo bora ni Kitabu cha Allaah, mwongozo bora ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), shari ya mambo ni yale yenye kuzuliwa na kila chenye kuzuliwa ni Bid´ah.”[3]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

 Kitendo hichi ni Bid´ah ambacho hakikufanywa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum). Kwa hiyo ni wajibu kuyaacha na kutubu kwa Allaah (Subhaanah) kwa yale yaliyotangulia. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ

“Tubuni kwa Allaah nyote, enyi waumini, mpate kufaulu.”[4]

وَإِنِّي لَغَفَّارٌ لِّمَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا ثُمَّ اهْتَدَىٰ

”Hakika Mimi ni Mwingi mno wa kusamehe kwa anayetubia na akaamini na akatenda mema kisha akaendelea kuongoka.”[5]

[1] al-Bukhaariy (2697), Muslim (1718), Abu Daawuud (4606), Ibn Maajah (14) na Ahmad (06/256).

[2] Muslim (1718).

[3] Muslim (867), an-Nasaa´iy (1578), Ahmad (03/371) na ad-Daarimiy (206).

[4] 24:31

[5] 20:82

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (30/44-46)
  • Imechapishwa: 11/09/2021