Ilipokuwa maneno ya Malaika (´alayhimus-Salaam) yanaashiria kuwa wao ni bora kuliko khalifa ambaye Allaah anataka kumweka ardhini, ndipo Allaah akataka kuwabainishia miongoni mwa fadhilah za Aadam jambo ambalo litawafanya kutambua ubora wake na ukamilifu wa hekima na ujuzi Wake Allaah:

وَعَلَّمَ آدَمَ الْأَسْمَاءَ كُلَّهَا ثُمَّ عَرَضَهُمْ عَلَى الْمَلَائِكَةِ فَقَالَ أَنبِئُونِي بِأَسْمَاءِ هَـٰؤُلَاءِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ قَالُوا سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا ۖ إِنَّكَ أَنتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ

“Akamfunza Aadam majina yote kisha akavionesha mbele ya Malaika ambapo akasema: “Niambieni majina ya hivi kama ni wakweli.” Wakasema: “Utakasifu ni Wako, hatuna sisi elimu isipokuwa Uliyotufunza; kwani hakika Wewe mjuzi wa yote, Mwingi wa hekima.”[1]

Alimfunza maneno ya vitu na akamfunza matamshi na maana yavyo mpaka vitu vikubwavikubwa na vidogovidogo.

ثُمَّ عَرَضَهُمْ عَلَى الْمَلَائِكَةِ

“… kisha akavionesha mbele ya Malaika… “

Akavidhihirisha vitu hivyo kwa Malaika kwa lengo la kuwapa mtihani kama watavijua au hawatovijua. Akasema:

أَنبِئُونِي بِأَسْمَاءِ هَـٰؤُلَاءِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ

“Niambieni majina ya hivi kama ni wakweli.”

katika maneno yenu na yale mliyofikiria ya kwamba nyinyi ni wabora kuliko khalifa huyu.

قَالُوا سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا

“Wakasema: “Utakasifu ni Wako, hatuna sisi elimu isipokuwa Uliyotufunza.”

Bi maana tunakutakasa kwa kule kupingana Nawe na kwenda kinyume na amri Yako. Sisi hatuna elimu kwa njia yoyote ile isipokuwa yale uliyotufunza – kutokana na fadhilah na ukarimu Wako.

إِنَّكَ أَنتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ

“Kwani hakika Wewe mjuzi wa yote, Mwingi wa hekima.”

Mjuzi ambaye ujuzi Wake umekizunguka kila kitu. Hakifichikani Kwake chochote kile kilicho na uzito wa chembe ndogo kabisa mbinguni na ardhini wala kilicho kidogo au kikubwa kuliko hivo.

Mwingi wa hekima ambaye yuko na hekima kamilifu ambazo viumbe hawatoki ndani yake na wala maamrisho hayapondoki nayo. Hakuumba wala kuamrisha kitu isipokuwa ni kutokana na hekima. Maana ya hekima ni kule kukiweka kitu mahali pake stahiki.

Kwa hiyo wakakubali na wakatambua ujuzi na hekima ya Allaah na upungufu wao wa kutambua kitu kidogo kabisa. Pia wametambua fadhilah za Allaah juu yao na kwamba amewafundisha mambo wasiyoyajua.

[1] 02:31-32

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-Kariym, uk. 39
  • Imechapishwa: 11/06/2020