Mzushi ni mbaya zaidi kuliko mtenda madhambi

Swali: Mtunzi wa kitabu ametumia Hadiyth kuhusu maasi kwa ajili ya kuthibitisha kuwa mtu wa Bid´ah anatakiwa kutengwa na asisalimiwe. Ni vipi amefikia jambo hilo?

Jibu: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumuitikia salamu ´Ammaar bin Yaasir kwa sababu tu ya kujitia manukato kwa zafarani. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumuitikia salamu bwana yule ambaye alikuja na huku amevaa mnyororo wa dhahabu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwaitikia salamu kikosi cha wale watu ambao walikuja na huku wamevaa hariri na pete za dhahabu. Yote hayo kwa sababu ya maasi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimsusa Zaynab bint Jahsh. Ni vipi tusiyatumie haya kuwakata wazushi? Ikiwa ni jambo la lazima kuwakata watenda maasi (pamoja na kwamba maasi ni mepesi zaidi kuliko Bid´ah) basi kuna umuhimu mkubwa zaidi kuwakata watu wa Bid´ah. Kwa sababu mzushi ni mbaya zaidi kuliko mtenda maasi. Mtenda maasi utamuona daima ni mwenye kuogopa juu ya dhambi zake, anaona aibu kuyataja na siku zote hutilia umuhimu wa kutubu na kujirudi. Lakini mtu wa Bid´ah hawezi kujirudi au kuona aibu juu ya Bid´ah zake. Hili ni jambo linalotambulika. Kwa hivyo ikiwa mtenda maasi anakatwa, basi mzushi ana haki zaidi ya kufanywa hivo.

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath-ur-Rahiym al-Waduud, uk. 253
  • Imechapishwa: 12/06/2020