59. Radd juu ya utata wa nne: “Namuomba Mtume (صَلَّى اللّٰهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم) kile alichopewa na Allaah”

Akisema: “Kwa hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kapewa uombezi na mimi naomba kile alichompa Allaah.” Jibu ni kuwa: “Ni kweli kuwa Allaah kampa uombezi, lakini amekukataza hili[1]. Kasema ”Msiombe yeyote pamoja na Allaah.”. Ikiwa utamuomba Allaah akupe uombezi wa Mtume, tii Kauli Yake:

فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

”Msiombe yeyote pamoja na Allaah.” (al-Jinn 72 : 18)

Isitoshe uombezi wamepewa wengine asiyekuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Imesihi ya kwamba Malaika wataombea, mawalii wataombea na watoto waliokufa kabla ya kubaleghe wataombea. Utasema ya kwamba: “Kwa vile Allaah kawapa uombezi hivyo nitaiomba kutoka kwao?” Ukisema hivyo, utakuwa umerejea katika kuwaabudu watu wema ambao Allaah kawataja katika Kitabu Chake. Na ukisema: “Hapana”, kauli yako inakuwa batili: “Allaah Kawapa uombezi na mimi ninaomba kile alichowapa Allaah.”

MAELEZO

Haina maana kwa vile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wengineo wamepewa uombezi itajuzu kuomba kutoka kwao ilihali wameshakufa. Dalili ya hilo ni kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amepinga yeyote kuombea mbele Yake isipokuwa baada ya idhini Yake na baada ya kumridhia yule muombewaji. Sababu nyingine ni kuwa kuomba uombezi kutoka kwa maiti ni shirki na Allaah ameharamisha shirki, kuyaharibu matendo ya mwenye kufanya hivo na kumharamishia Pepo.

Allaah (Subhaanah) amewakemea wale wanaomuomba asiyekuwa Yeye na kusema kwamba [wanaowaomba] ni waombezi wao mbele ya Allaah. Allaah amejitakasa kutokamana na hilo na akaliita kuwa ni shirki.

Isitoshe Allaah hakumpa uombezi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) peke yake. Je, kila aliyepewa uombezi utaomba uombezi kutoka kwake kama walivyokuwa wakifanya washirikina wa hapo mwanzo:

وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Na wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”” (10:18)

[1] yaani kumuomba mwengine asiyekuwa Yeye.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 88
  • Imechapishwa: 20/01/2017