53. Radd juu ya utata wa pili: kuwaomba watu wema sio shirki

Ama jibu la kina

Kwa hakika maadui wa Allaah wana vipingamizi vingi dhidi ya dini ya Mitume [vipingamizi] ambavyo wanawazuia kwavyo watu. Katika maneno yao ni pamoja na kusema kwao: “Sisi hatumshirikishi Allaah, bali sisi tunashuhudia ya kwamba hakuna mwenye kuumba, wala hakuna mwenye kuruzuku, wala hakuna mwenye kunufaisha na kudhuru isipokuwa Allaah Mmoja pekee hali ya kuwa hana mshirika, na kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hamiliki katika nafsi yake si manufaa wala madhara, tusiseme ´Abdul-Qaadir au mwengine yeyote. Lakini mimi ni mwenye kufanya madhambi na hawa watu wema wana jaha mbele ya Allaah na hivyo ninamuomba Allaah kwa kupitia kwao. Mjibu kwa yaliyotangulia, nayo ni: “Wale ambao Mtume wa Allaah aliwapiga vita walikuwa wanakubali hayo uliyoyataja na walikuwa wakikubali ya kwamba waungu wao wa batili hawaendeshi kitu, isipokuwa tu walichokuwa wanataka ni jaha na uombezi.”

Msomee aliyoyataja Allaah katika Kitabu Chake na akayaweka wazi. Akikwambia: “Aayah hizi ziliteremshwa kwa wale waliokuwa wanaabudu masanamu! Vipi mtawafanya watu wema ni kama masanamu? Au vipi mtawafanya Mitume ni kama masanamu?” Mjibu kama ilivyotangulia. Hivyo, ikiwa atakubali ya kwamba makafiri wanashuhudia kuwa Rubuubiyyah yote ni ya Allaah, na kwamba hawakutaka chochote kutoka kwao zaidi isipokuwa uombezi tu, lakini anachotaka ni kutofautisha baina ya kitendo chao na kitendo chake kwa aliyoyataja, mkumbushe ya kwamba miongoni mwa makafiri kulikuwa wanaoabudu masanamu, watu wema na masanamu, wengine wakiwaabudu mawalii. Allaah amesema kuhusu wao:

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يَدْعُونَ يَبْتَغُونَ إِلَىٰ رَبِّهِمُ الْوَسِيلَةَ أَيُّهُمْ أَقْرَبُ

”Hao wanaowaomba wao wenyewe wanatafuta kwa Mola wao njia ya kujikurubisha na kujikurubisha Kwake kadri na wanavyoweza.” (al-Israa´ 17 : 57)

Na wanamuomba ´Iysa bin Maryam na mama yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

مَّا الْمَسِيحُ ابْنُ مَرْيَمَ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِ الرُّسُلُ وَأُمُّهُ صِدِّيقَةٌ ۖ كَانَا يَأْكُلَانِ الطَّعَامَۗ انظُرْ كَيْفَ نُبَيِّنُ لَهُمُ الْآيَاتِ ثُمَّ انظُرْ أَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ قُلْ أَتَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَمْلِكُ لَكُمْ ضَرًّا وَلَا نَفْعًا ۚ وَاللَّـهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ

”al-Masiyh, mwana wa Maryam, si chochote isipokuwa ni Mtume tu, bila shaka wamekwishapita kabla yake Mitume wengine na mama yake alikuwa mkweli sana. Wote wawili walikuwa wanakula. Tazama jinsi Tunavyowabainishia Aayah – kisha tazama vipi wanavyogeuzwa!” Sema: “Vipi mnaabudu asiyekuwa Allaah asiyemiliki kukudhuruni wala kukunufaisheni? Allaah ndiye Mwenye kusikia yot, Mjuzi wa yote.” (al-Maaidah 05 : 75-76)

Mtajie Kauli Yake (Ta´ala):

وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا ثُمَّ يَقُولُ لِلْمَلَائِكَةِ أَهَـٰؤُلَاءِ إِيَّاكُمْ كَانُوا يَعْبُدُونَ قَالُوا سُبْحَانَكَ أَنتَ وَلِيُّنَا مِن دُونِهِم ۖ بَلْ كَانُوا يَعْبُدُونَ الْجِنَّ ۖ أَكْثَرُهُم بِهِم مُّؤْمِنُونَ

”Na siku Atakayowakusanya wote kisha atawaambia Malaika: “Je, hawa ndio waliokuwa wakikuabuduni nyinyi?” Watasema: “Umetakasika! Wewe ndiye Mlinzi wetu na tunajitena mbali na wao. Bali walikuwa wakiabudu majini ambao wengi wao wakiwaamini.” (Saba´ 34 : 40-41)

Na Kauli Yake (Ta´ala):

وَإِذْ قَالَ اللَّـهُ يَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ أَأَنتَ قُلْتَ لِلنَّاسِ اتَّخِذُونِي وَأُمِّيَ إِلَـٰهَيْنِ مِن دُونِ اللَّـهِ ۖ قَالَ سُبْحَانَكَ مَا يَكُونُ لِي أَنْ أَقُولَ مَا لَيْسَ لِي بِحَقٍّ إِن كُنتُ قُلْتُهُ فَقَدْ عَلِمْتَهُ ۚ تَعْلَمُ مَا فِي نَفْسِي وَلَا أَعْلَمُ مَا فِي نَفْسِكَ ۚ إِنَّكَ أَنتَ عَلَّامُ الْغُيُوبِ

”Na Allaah atakaposema: “Ee ‘Iysaa, mwana wa Maryam! Je, wewe ndiye uliwaambia watu: “Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni miungu miwili badala ya Allaah?” Atasema: “Utakaso ni Wako! Vipi nitasema yale yasiyo kuwa haki kwangu? ikiwa nimesema hayo basi Ungeliyajua. Unayajua yale yote yaliyomo ndani ya nafsi yangu na wala mimi sijui yale yaliyomo ndani ya Nafsi Yako; hakika Wewe ni Mjuzi yote yaliyojificha.”” (al-Maaidah 05 : 116)

Mwambie: “Umejua sasa ya kwamba Allaah amemkufurisha yule aliyeyaabudu masanamu na watu wema na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawapiga vita?” Ikiwa atasema: “Makafiri walikuwa wanataka [manufaa na madhara] kutoka kwao ilihali mimi ninashuhudia ya kwamba Allaah ndiye Mwenye kunufaisha, Mwenye kudhuru na Mwendeshaji wa mambo. Sitaki [manufaa na madhara] isipokuwa tu kutoka Kwake. Watu wema hawana katika hilo lolote, lakini ninawaomba kwa kuwa natarajia kutoka kwa Allaah uombezi wao.” Jibu ni kuwa, maneno haya na yale ya makafiri ni sawa sawa. Msomee Kauli Yake (Ta´ala):

وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

“Na wale waliojichukulia badala Yake walinzi [wakisema]: “Hatuwaabudu isipokuwa kwa lengo la kutukurubisha kwa Allaah karibu.”” (az-Zumar 39 : 03)

Kauli Yake (Ta´ala):

وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

”Na wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”” (Yuunus 10 : 18)

Jua ya kwamba shubuha hizi tatu ndio kubwa walizonazo. Pale utapojua kuwa Allaah katuwekea nazo wazi katika Kitabu Chake na ukazifahamu vizuri, yaliyo baada yake yatakuwa sahali zaidi kuliko hayo.

MAELEZO

Shaykh (Rahimahu Allaah) katika kipande hichi ametaja shubuha tatu za washirikina ambao ndio utata wao muhimu zaidi. Ukiweza kuzijibu vizuri basi yaliyo baada yake ni mepesi zaidi kuliko hizi.

Utata wa kwanza wanasema ya kwamba wao wanashuhudia kuwa hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba wanatambua kuwa hakuna anayedhuru wala kunufaisha isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hamiliki manufaa wala madhara, sembuze ´Abdul-Qaadir al-Jaylaaniy. Lakini hata hivyo wanasema kuwa watu hawa wana haja mbele ya Allaah na hivyo wao eti wanaiomba kutoka kwa Allaah kupitia wao. Kwa msemo mwingine wanachotaka kusema ni kwamba wanawafanya kuwa wakati kati baina yao na Allaah kutokana na ule ubora walionao. Jibu ni lepesi sana kutoka katika Qur-aan. Unatakiwa uwaambie ya kwamba washirikina – kwa sampuli zao mbalimbali – hawakuwa wakiitakidi [juu ya waungu wao] ya kwamba wanaumba, wanaruzuku, wananufaisha na kudhuru. Si vinginevyo isipokuwa tu waliwafanya kuwa ni wakati kati baina yao na baina ya Allaah, jambo ambalo Ameitakasa nafsi Yake kutokamana na matendo yao na akayaita kuwa ni shirki pamoja na kwamba wao wanasema kuwa ni waombezi wao mbele ya Allaah na wanaitakidi kuwa hawanufaishi na wala hawadhuru. Kwa msemo mwingine walichokusudia ni kufungamana na jaha peke yake. Kwa hivyo Aayah zinathibitisha ya kwamba washirikina walikuwa wakitambua ya kwamba hakuna Mwenye kuumba, Mwenye kuruzuku na Mwenye kuyaendesha mambo isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) peke yake na kwamba masanamu na waungu wao hawaumbi, hawaruzuku na wala hawaendeshi mambo pamoja na Allaah. Walichofanya tu ni kuwachukua kuwa wakati na kati. Hivyo basi, hakuna tofauti kati yenu na wao.

Ikiwa wewe una madhambi ni kwa nini usimuombe Allaah msamaha na ukatubu kwa Allaah? Allaah (Jalla wa ´Alaa) amekuamrisha kuomba msamaha na akakuahidi kukusamehe na kukubali kutoka kwako na kukusamehe madhambi yako. Hakukwambia endapo utafanya dhambi nenda kwenye kaburi la walii fulani au mja mwema fulani na utawasali kwake na umfanye kuwa ni mkati kati baina yangu na baina yako.

Mwambie vilevile ya kwamba watu hawa ikiwa kweli wana jaha mbele ya Allaah, basi hakika jaha yao ni yao na wema wao ni wao na wewe huna jengine isipokuwa matendo yako tu. Wema wa watu wema na jaha yao mbele ya Allaah ni vyao na wewe huna mafungamano yoyote na jaha na wema wao. Hayo hayatokufaa kitu ikiwa ni mtenda madhambi. Haya yanahusu hata baba yako na mtu aliye karibu zaidi na wewe kama baba yako. Hata kama atakuwa ni miongoni mwa watu wema kabisa hawezi kukufaa kitu:

يَوْمَ لَا تَمْلِكُ نَفْسٌ لِّنَفْسٍ شَيْئًاۖ وَالْأَمْرُ يَوْمَئِذٍ لِّلَّـهِ

“Siku ambayo nafsi yoyote haitoimilikia nafsi nyingine kitu chochote na amri Siku hiyo ni ya Allaah pekee.” (82:19)

كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ رَهِينَةٌ

“Kila nafsi iko katika rehani kwa yale iliyoyachuma.” (74:38)

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمْ وَاخْشَوْا يَوْمًا لَّا يَجْزِي وَالِدٌ عَن وَلَدِهِ وَلَا مَوْلُودٌ هُوَ جَازٍ عَن وَالِدِهِ شَيْئًا

“Enyi watu! Mcheni Mola wenu na iogopeni Siku ambayo mzazi hatomfaa mwana wake na wala mwana hatomfaa mzazi wake chochote.” (31:33)

يَوْمَ يَفِرُّ الْمَرْءُ مِنْ أَخِيهِ وَأُمِّهِ وَأَبِيهِ وَصَاحِبَتِهِ وَبَنِيهِ

“Siku mtu atakapomkimbia ndugu yake na mama yake na baba yake na mkewe na wanawe.” (80:34-36)

Utata wa pili ukimsomea maneno Yake (Ta´ala):

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Wanaabudu badala ya Allaah visivyowadhuru wala kuwanufaisha na wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”” (10:18)

أَلَا لِلَّـهِ الدِّينُ الْخَالِصُ ۚ وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

“Tanabahi! Ni ya Allaah pekee dini iliyotakasika. Na wale waliojichukulia badala Yake walinzi [husema]: “Hatuwaabudu isipokuwa ili watukurubishe kwa Allaah ukaribio.” (39:03)

na ukambainishia kuwa washirikina hawakutaka jengine kutoka kwa waungu wao isipokuwa uombezi tu na yeye akakujibu ya kwamba Aayah hizi zimeteremka juu ya wale wenye kuyaabudu masanamu na kwamba yeye haabudu masanamu na kuwa anatawasali Kwake kupitia waja wema – ni vipi utawafanya watu wema kuwa ni masanamu? Jibu juu ya haya ni lepesi sana. Mambo ni kwamba Allaah ametaja kuwa washirikina kuna ambao walikuwa wakiyaabudu masanamu, wengine wakiwaabudu mawalii na wengine wakiwaabudu waja wema. Allaah aliwasawazisha baina yao katika hukumu na wewe unataka kutofautisha kati yao kwa kudhani kwamba kuyaabudu masanamu haifai tofauti na watu wema ambao inafaa endapo lengo la mtu itakuwa ni Tawassul! Dalili ya hili ni kwamba Allaah ametaja aina mbalimbali za washirikina. Katika wao kuna waliokuwa wakiabudu watu wema. Amesema (Ta´ala):

وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا ثُمَّ يَقُولُ لِلْمَلَائِكَةِ أَهَـٰؤُلَاءِ إِيَّاكُمْ كَانُوا يَعْبُدُونَ قَالُوا سُبْحَانَكَ أَنتَ وَلِيُّنَا مِن دُونِهِم ۖ بَلْ كَانُوا يَعْبُدُونَ الْجِنَّ ۖ أَكْثَرُهُم بِهِم مُّؤْمِنُونَ

”Na siku Atakayowakusanya wote kisha atawaambia Malaika: “Je, hawa ndio waliokuwa wakikuabuduni nyinyi?” Watasema: “Umetakasika! Wewe ndiye Mlinzi wetu na tunajitena mbali na wao. Bali walikuwa wakiabudu majini ambao wengi wao wakiwaamini.” (34:40-41)

Siku ya Qiyaamah Allaah (Jalla wa ´Alaa) atawauliza Malaika ilihali Yeye (Subhanaahu wa Ta´ala) ni mjuzi zaidi. Lakini hata hivyo atawauliza ili kubatilisha hoja ya watu hawa:

أَهَـٰؤُلَاءِ إِيَّاكُمْ كَانُوا يَعْبُدُونَ

“Je, hawa ndio waliokuwa wakikuabuduni nyinyi?”

Ni dalili inayothibitisha kuwa katika wao kuna waliokuwa wakiwaabudu Malaika lakini hata hivyo Malaika watajitenga nao siku ya Qiyaamah na kuwakana kwamba hawakuwaamrisha kufanya hivo na wala hawakuridhia kitendo hicho:

سُبْحَانَكَ أَنتَ وَلِيُّنَا مِن دُونِهِم ۖ بَلْ كَانُوا يَعْبُدُونَ الْجِنَّ

“Umetakasika! Wewe ndiye Mlinzi wetu na tunajitena mbali na wao. Bali walikuwa wakiabudu majini.”

Bi maana mashaytwaan ndio waliokuwa wakiwaamrisha kuwaabudu Malaika. Kwa kuwa Malaika hawaamrishi jengine isipokuwa kumuabudu Allaah pekee:

وَمَن يَقُلْ مِنْهُمْ إِنِّي إِلَـٰهٌ مِّن دُونِهِ فَذَٰلِكَ نَجْزِيهِ جَهَنَّمَ ۚ كَذَٰلِكَ نَجْزِي الظَّالِمِينَ

“Yeyote yule miongoni mwao atakayesema: “Mimi ni mungu badala Yake,” basi huyo Tutamlipa [Moto wa] Jahannam – hivyo ndivyo Tunavyowalipa madhalimu.”” (21:29)

Ni dalili inayofahamisha kwamba katika wao kuna ambao walikuwa wakiwaabudu Malaika. Malaika ndio viumbe wema kabisa. Amesema (Ta´ala) kuhusu wao:

لَا يَسْبِقُونَهُ بِالْقَوْلِ وَهُم بِأَمْرِهِ يَعْمَلُونَ

“Hawamtangulii kwa neno – nao kwa amri Yake wanafanya.” (21:27)

Vilevile kuna ambao walikuwa wakiwaabudu Mitume na waja wema kama mfano wa al-Masiyh, mwana wa Maryam, na mama yake. Kutawasali kwa Malaika na Mitume na pia kuwaomba badala ya Allaah kukibatilika basi kumebatilika vilevile kutawasali kwa waja wema wengine na kuwaomba badala ya Allaah. Amesema (Ta´ala):

أَلَا لِلَّـهِ الدِّينُ الْخَالِصُ ۚ وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ إِنَّ اللَّـهَ يَحْكُمُ بَيْنَهُمْ فِي مَا هُمْ فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي مَنْ هُوَ كَاذِبٌ كَفَّارٌ

“Tanabahi! Ni ya Allaah pekee dini iliyotakasika. Na wale waliojichukulia badala Yake walinzi [husema]: “Hatuwaabudu isipokuwa ili watukurubishe kwa Allaah ukaribio.” Hakika Allaah atahukumu baina yao katika yale waliyokhitilafiana. Hakika Allaah hamwongoi ambaye ni muongo kafiri.” (39:03)

Kwa kuwa lililo wajibu ni kumtakasia ´ibaadah Allaah pekee (´Azza wa Jall). Inahusiana na ´ibaadah sampuli zote kukiwemo du´aa, kuchinja, nadhiri na nyinginezo. Mwenye kuchinja na akamuomba asiyekuwa Allaah basi huyo ni mshirikina aliyetoka katika Uislamu.

Utata wa tatu akikubali kuwa kumuomba asiyekuwa Allaah ni shirki lakini hata hivyo akasema kuwa yeye hamuombi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala mwengine na kwamba hayo ayafanyayo sio kuwaomba bali ni kutaka uombezi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – je, wewe unapinga uombezi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Hapo wewe utakuwa umeingia naye katika mzozo na utata mwingine. Nao ni kwamba kule kumuomba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumtaka msaada amekuita kuwa ni kutaka uombezi na hakuita kuwa ni maombi na kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amepewa uombezi na kwamba eti yeye anaomba uombezi aliyopewa. Mjibu na kumwambia kwamba wewe hupingi uombezi bali unakubali kuwa uombezi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni haki na kwamba yeye ndiye muombezi na mwenye kuitikiwa uombezi. Mwambie kuwa hayo huyapingi lakini hata hivyo uombezi hauombwi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilihali ameshakufa. Kinachotakiwa ni kuuomba kutoka kwa Allaah kwa kuwa maombezi yote ni milki ya Allaah (´Azza wa Jall). Allaah (Ta´ala) amesema:

قُل لِّلَّـهِ الشَّفَاعَةُ جَمِيعًا ۖ لَّهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ

”Sema: “Uombezi wote ni wa Allaah pekee. Yeye ndiye ana ufalme wa mbingu na ardhi.”” (39:44)

Aina zote za maombezi ni milki ya Allaah. Midhali aina zote za maombezi ni milki ya Allaah basi haziombwi isipokuwa kutoka kwa Yule Anayezimiliki ambaye si mwengine ni Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hamiliki uombezi na wala hakuna yeyote anayemiliki uombezi isipokuwa baada ya idhini ya Allaah. Uombezi ni milki ya Allaah (´Azza wa Jall).

Isitoshe jengine ni kwamba uombezi hautowafaa watu wote. Utawafaa watu wa Tawhiyd peke yake tofauti na yeye ambaye si katika watu wa Tawhiyd. Sababu ni kuwa anamuomba asiyekuwa Allaah. Uombezi una sharti mbili:

Ya kwanza: Kuiomba kutoka kwa Allaah na isiombwe kutoka kwa mwengine.

Ya pili: Yule mwenye kuombewa awe ni katika watu wa Tawhiyd na asiwe ni katika watu wa shirki na kufuru. Dalili ya sharti ya pili ni maneno Yake (Ta´ala):

وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ

“… na wala hawamuombei uombezi yeyote isipokuwa yule ambaye Amemridhia.” (21:28)

Haridhii isipokuwa mtu wa Tawhiyd peke yake. Dalili ya sharti ya kwanza ni maneno Yake (Ta´ala):

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

“Nani huyu awezaye kuombea mbele Yake bila ya idhini Yake?” (02:255)

Inahusu Malaika, Mitume, mawalii na waja wote wema. Hakuna yeyote atayeombea mbele Yake isipokuwa baada ya Allaah kumuadhinisha:

وَكَم مِّن مَّلَكٍ فِي السَّمَاوَاتِ لَا تُغْنِي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا إِلَّا مِن بَعْدِ أَن يَأْذَنَ اللَّـهُ لِمَن يَشَاءُ وَيَرْضَىٰ

“Malaika wangapi mbinguni hautowafaa kitu chochote uombezi wao isipokuwa baada ya kuwa Allaah ametolea idhini kwa amtakaye na akaridhia.” (53:26)

Kwa hivyo usiombe uombezi kutoka kwa viumbe maiti. Unachotakiwa ni wewe kuomba uombezi kutoka kwa Allaah kwa kusema:

“Ee Allaah! Nifanye nipate uombezi wa Mtume Wako.”

Usiiombe kutoka kwa maiti. Haya unayosema kuhusu kuomba uombezi ndio ambayo Allaah amewakafirisha kwayo washirikina. Washirikina walipoomba kinga kwa mawalii, watu wema, Malaika na Mitume na kuwaomba uombezi Allaah aliwakufurisha kwa hilo na kusema (Ta´ala):

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِۚ قُلْ أَتُنَبِّئُونَ اللَّـهَ بِمَا لَا يَعْلَمُ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ

“Wanaabudu badala ya Allaah visivyowadhuru wala kuwanufaisha na wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.” Sema: “Je, mnamjulisha Allaah kwa yale asiyoyajua katika mbingu na ardhini? Utakasifu ni Wake na yuko juu kabisa kwa yale yote wanayomshirikisha.”” (10:18)

Haya unayosema ndio ambayo Allaah amewakufurisha kwayo washirikina. Nayo si mengine ni kuwaabudu mawalii na watu wema na pia kuwaomba uombezi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 74-80
  • Imechapishwa: 05/01/2017