5- Miongoni mwa matunda ya elimu ni tabia njema. Ni kipi kitakujuza ni nini tabia njema? Ni matunda makubwa. Hakika elimu inaitengeneza tabia ya muislamu. Tabia ndio kitu kikubwa ambacho muislamu anaweza kujichumia. Muislamu hawezi kuchuma kitu kikubwa baada ya imani kama tabia njema.

Mwanafunzi anatakiwa azinduke juu ya tunda hili na aifanye elimu ni yenye kuitengeneza tabia yake. Kwa hivyo awe ni mwenye kuwatendea wema wazazi wake, kuwaunga ndugu zake, kutangamana vyema na watu, kutangamana vyema na familia yake na awe na matangamano mazuri na mke wake.

Miongoni mwa mambo yanayosikitisha ni kuwa baadhi ya wanafunzi wamesababisha kutoa sura mbaya kwa kutafuta elimu. Utamuona nyumbani kwake ni miongoni mwa watu wenye tabia mbaya kabisa kwa familia yake. Utamuona anapotangamana na wazazi wake ni miongoni mwa watu wenye kutangamana nao vibaya kabisa. Anapoombwa kitu anasema: “[Siwezi] mimi hivi sasa nina darsa.” Anapoombwa amfikishe sehemu fulani anasema: “[Siwezi] hivi sasa nina miadi na marafiki zangu.” Anapoombwa kitu anasema: “Nina hili na lile.” Haya yamewafanya baadhi ya wazazi hawatamani wana wao wawe ni katika wanafunzi.

Baadhi ya wanafunzi hazitambui haki za wazazi wao. Anamsusa na muda wake mwingi anakuwa na marafiki zake katika mizunguko ya kielimu. Hajui kujipangia wakati wake na hajui ni muda gani mke wake anatakiwa kuwa pamoja nae. Anapoingia nyumbani kwake anakuwa kama simba. Pepo yake ni kwa marafiki zake na moto wake ni kwa mke wake ambapo hazungumzi. Tabasamu, uso wenye bashasha na furaha wanaipata marafiki na ndugu zake. Hili halina shaka ya kwamba ni katika makosa makubwa. Mwanafunzi anatakiwa aifanye elimu ni yenye kumtengenezea tabia njema. as-Salaf as-Swaalih walikuwa ni kiigizo chema katika hili. Mpaka Imaam Ahmad alikuwa akisema:

“Lau dunia mzima ingelikuwa ni tonge na nikampa nalo ndugu yangu isingelikuwa israfu.”[1]

Hii ni tabia njema. as-Salaf as-Swaalih walikuwa ni kiigizo chema inapokuja katika tabia njema.

Wanafunzi wanatakiwa wafaidi kutoka katika elimu yao tabia njema na wawe ni kama Qur-aan inayotembea kati ya watu. Watu wakiwaona waseme:

“Elimu inamfanya mtu namna hii.”

Wanatakiwa pindi mtu atapomuona mwanafunzi aseme kuwaambia wanawe:

“Kuweni kama huyu.”

Hivi ndivyo walivyokuwa as-Salaf as-Swaalih.

[1] Twabaqaat-ul-Hanaabilah” (01/106) ya Ibn Abiy Ya´laa.

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliymillaah ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Ilm wa Wasaaailuh wa Thimaaruh
  • Imechapishwa: 22/10/2016