21. Ahl-us-Sunnah wanawapenda na kuwaheshimu Maswahabah wote

Abu Muhammad ´Abdur-Rahmaan bin Abiy Haatim amesema:

4- Mtu bora wa Ummah huu baada ya Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Abu Bakr as-Swiddiyq, ´Umar bin al-Khattwaab, ´Uthmaan bin ´Affaan na ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anhum). Wao ndio makhaliyfah waongofu.

MAELEZO

Miongoni mwa ´Aqiydah na misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kuwaheshimu Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kuwapenda na kuitakidi kuwa wao ni bora kuliko ummah mzima walobaki. Allaah awawie radhi! Ibn Abiy Haatim amesema:

“Mtu bora wa Ummah huu baada ya Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Abu Bakr asw-Swiddiyq… “

Ahl-us-Sunnah hawana shaka juu ya hili. Hata Khawaarij vilevile wanaitakidi kuwa Abu Bakr na ´Umar ndio bora, wanamchukia ´Uthmaan, ´Aliy na wengine. Ahl-us-Sunnah ni wenye kuzunguka na haki na dalili – himdi zote anastahiki Allaah. Wanajua ni hadhi gani walionayo Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanatambua kuwa wanatofautiana katika fadhila na kwamba baadhi ni bora kuliko wengine, kama ilivyosihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qurrat-ul-´Aynayn bi Tawdhwiyh Ma´aaniy ´Aqiydat-ir-Raaziyayn, uk. 34-35
  • Imechapishwa: 15/10/2016