22. Mtu bora baada ya Manabii na Mitume

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema wazi juu ya fadhila za Abu Bakr:

“Katika watu walionifanyia wema mkubwa katika usuhubiano wao na mali yao ni Abu Bakr. Lau ningelichagua kipenzi wa hali ya juu mbali na Mola wangu basi ningelimchagua Abu Bakr, lakini kubaki udugu na mapenzi ya Kiislamu.” al-Bukhaariy (3654).

Maswahabah watatu wamesimulia fadhila hii juu ya Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) na imepokelewa vilevile na al-Bukhaariy na Muslim.

Mapenzi haya ndio aina kubwa kabisa ya mapenzi. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa hana nayo kwa mwengine asiyekuwa Mola wake (Subhaanahu wa Ta´ala). Yeye ndiye anayetakiwa kupendwa mapenzi ya hali ya juu. Kadhalika Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akimpenda Mola wake mapenzi ya hali ya juu yasiyokuwa na mfano.

Hadiyth inatilia ngubu ubora wa Abu Bakr juu ya Maswahabah wengine wote (Radhiya Allaahu ´anhum) kwa mitazamo miwili: Wa kwanza:

“Katika watu walionifanyia wema mkubwa katika usuhubiano wao na mali yao ni Abu Bakr.”

Wa pili:

“Lau ningelichagua kipenzi wa hali ya juu mbali na Mola wangu basi ningelimchagua Abu Bakr… “

Ni dalili inayothibitisha kuwa yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimpa kipaumbele Abu Bakr juu ya wengine wote. Ni dalili ya wazi ya kwamba Abu Bakr ni bora kuliko ´Umar na Maswahabah wengine wote waliosalia (Radhiya Allaahu ´anhum). Yeye ndiye mtu bora baada ya Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Baada ya Manabii na Mitume anakuja Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anhum). Kwa mujibu wa maoni fulani yeye ndiye wa kwanza kuingia katika Uislamu. Alijitolea nafsi na mali yake kwa ajili ya kuunusuru Uislamu wakati ambapo wengine wote walikuwa wamemkosesha nusura Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akamwacha huru Bilaal (Radhiya Allaahu ´anh) na wengineo. Alijitolea nafsi yake na mali yake kwa ajili ya kuunusuru Uislamu. Kwa ajili hiyo anastahiki ngazi hii.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qurrat-ul-´Aynayn bi Tawdhwiyh Ma´aaniy ´Aqiydat-ir-Raaziyayn, uk. 35-36
  • Imechapishwa: 15/10/2016