06. Kila mtu anapata kile anachostahiki

Ikiwa kila kitu kinatokamana na utashi wa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) na anaendesha mambo yote, mtu afanye nini? Mtu ashike njia ipi ikiwa Allaah (Ta´ala) amemkadiria kuwa atapotea na hatoongoka? Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) anamwongoza yule ambaye anastahiki uongofu kama ambavyo anampoteza yule ambaye anastahiki kupotezwa. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

فَلَمَّا زَاغُوا أَزَاغَ اللَّـهُ قُلُوبَهُمْ

“Basi walipopotoka, Allaah akapotosha nyoyo zao.”[1]

فَبِمَا نَقْضِهِم مِّيثَاقَهُمْ لَعَنَّاهُمْ وَجَعَلْنَا قُلُوبَهُمْ قَاسِيَةًۖ يُحَرِّفُونَ الْكَلِمَ عَن مَّوَاضِعِهِ ۙوَنَسُوا حَظًّا مِّمَّا ذُكِّرُوا بِهِ

“Kwa baadaye walivunja ahadi zao, Tuliwalaani na tukazifanya nyoyo zao kuwa ngumu. Wanayapotosha maneno [Kitabu cha Allaah] kutoka mahali pake na wakasahu sehemu ya yale waliyokumbushwa kwayo.”[2]

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amebainisha kuwa anampoteza mja kwa kuwa yeye mwenyewe ndiye kasababisha hivo. Kama tulivyotangulia kusema mja hajui kile Allaah (Ta´ala) alichomkadiria. Hajui kama Allaah (Ta´ala) amemkadiria awe mpotevu au awe mwongofu. Ni vipi atashika njia ya upotevu na kutumia hoja kuwa Allaah (Ta´ala) ndiye kampangia hivo? Ni kwa nini asishike njia ya uongofu na kusema kuwa Allaah (Ta´ala) ametaka kumwongoza njia iliyonyooka? Hivi ni sawa kweli mtu akawa Jabriy wakati wa upotevu, na Qadariy wakati wa utiifu? Hapana, si sawa mtu akawa Jabriy wakati wa upotevu na maasi. Anapoenda kombo au akamuasi Allaah anasema kuwa ni kitu alikuwa ameshapangiwa na kwamba hawezi kutoka nje ya kitu Allaah alichokipanga na kukikadiria. Na pindi Allaah anapomwongoza katika utiifu na akamuwafikisha uongofu, anasema kuwa hiyo ni kazi yake mwenyewe. Kisha anadhani kuwa amemfanyia huduma Allaah na kusema kuwa amefanya hilo kutoka kwake mwenyewe. Anakuwa ni Qadariy inapokuja katika utiifu, Jabriy inapokuja katika maasi. Hili ni jambo haliwezekani.

[1] 61:05

[2] 05:13

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Qadhwaa’ wal-Qadar, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (5/220-221)
  • Imechapishwa: 25/10/2016