07. Fanya bidii ya maisha ya Aakhirah kama unavyofanya bidii ya maisha haya

Uhakika wa mambo ni kuwa mtu ana uwezo na utashi. Uongofu si jambo lililofichikana kama riziki na masomo. Kila mtu anajua kuwa riziki yake ameshakadiriwa. Pamoja na hivyo anapiganisha riziki hiyo ndani ya mji wake na nje ya mji wake, upande wa kulia na wa kushoto. Hakai nyumbani kwake na kusema:

“Ikiwa nimeshapangiwa riziki basi itanijia kwa hali yoyote.”

Bali anafanya bidii kutafuta riziki pamoja na kuwa bidii hiyo imefungamanishwa na kitendo. Imethibiti katika Hadiyth iliyosimuliwa na Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Kila mmoja wenu linakusanywa umbile lake kwenye tumbo la mama yake kwa muda wa siku arubaini. Kisha linakuwa kipande cha nyama kwa muda kama huo. Kisha inakuwa kipande cha mifupa kwa muda kama huo. Halafu anatumiwa Malaika anayeamrishwa kuandika mambo mane; riziki yake, muda wake wa kueshi, matendo yake na kama atakuwa ni mla khasara au mwenye furaha.”

Riziki imeandikwa kama ambavyo matendo mazuri na mabaya yameandikwa. Kwa nini unafanya kila uliwezalo kwa ajili ya kutafuta riziki ya dunia hii lakini hufanyi matendo mema ili uweze kuingia Peponi? Mbona ni jambo moja. Hakuna tofauti kati ya hayo mawili. Unafanya bidii kwa ajili ya riziki yako na maisha yako na unafanya kila uliwezalo ili uweze kuishi maisha marefu. Unapokuwa mgonjwa unaizunguka dunia nzima kwa ajili ya kumpata daktari hodari awezaye kukuponya. Pamoja na hivyo hutoishi muda mrefu zaidi ya vile ulivyokadiriwa. Maisha yako hayatozidi na wala hayatopungua. Hutotegemea makadirio na kusema:

“Nabaki nyumbani. Kama Allaah ameshanipangia kuwa nitaishi zaidi basi itakuwa hivo.”

Utafanya bidii zote ili kuweza kumpata daktari hodari awezaye kukuponya kwa idhini ya Allaah. Kwa nini hufanyi vivyo hivyo kwa ajili ya maisha ya Aakhirah na kwa ajili ya matendo mema?

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Qadhwaa’ wal-Qadar, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (5/221)
  • Imechapishwa: 25/10/2016