06. Hukumu ya kulitembelea kaburi la Nabii Yuunus

Swali: Katika kipindi kilichopita cha barnamiji hii umesema haifai kuyatembelea makaburi na kwamba ni katika kumshirikisha Allaah. Je, kumtembelea Nabii Yuunus na Nabii Jarjaysh kunaingia ndani ya makatazo hayo? Je, haifai kuswali maeneo hapo?

Jibu: Kuna aina mbili ya kuyatembelea makaburi:

1 – Matembezi yanayokubalika katika Shari´ah.

2 – Matembezi ya kizushi na ya kishirki.

Kuhusu matembezi yanayokubalika katika Shari´ah ni jambo limesuniwa katika makaburi ya waja wema na waislamu wote. Kukitambulika lilipo kaburi la Mtume yeyote – kama linalotambulika lilipo kaburi la Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – basi imesuniwa kulitembelea pasi na kulifungia safari. Haifungwi safari kwa ajili ya kuyatembelea makaburi. Safari haifungwi isipokuwa kuiendea misikiti mitatu; msikiti Mtakatifu, msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na msikiti wa al-Aqswaa. Misikiti hii mitatu ndio inafaa kuifungia safari. Kuhusu makaburi hayafungiwi safari. Lakini mtu akiwa ndani ya mji na akatumia fursa ya kuyatembelea imependekezwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yatembeleeni makaburi. Kwani hakika yanakukumbusheni Aakhirah.”[1]

Katika tamko lingine imekuja:

“Yatembeleeni makaburi. Kwani hakika yanakukumbusheni kifo.”

Jambo hilo limefanywa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum wa ardhwaahum).

Kwa hivyo muislamu akiyatembelea makaburi ya waislamu mjini mwake ambapo akawaombea du´aa na msamaha, basi huko kunazingatiwa ni kujikurubisha na tendo jema. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwafunza Maswahabah zake pindi wanapoyatembelea makaburi waseme:

السلام عليكم أهل الديار من المؤمنين والمسلمين وإنا إن شاء الله بكم لاحقون نسأل الله لنا ولكم العافية يرحم الله المستقدمين منا والمستأخرين

“Amani ya Allaah iwe juu yenu wakazi waumini na waislamu. Nasi – Allaah akitaka – tutaungana na nyinyi. Tunamuomba Allaah juu yetu sisi na nyinyi afya. Allaah amrehemu aliyetangulia katika sisi na atakayekuja baadaye.”[2]

Hivi ndivo alivowafunza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yeye mwenyewe (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiyatembelea makaburi, akiwaombea du´aa na msamaha wafu na akisema:

السلام عليكم دار قوم مؤمنين وإنا إن شاء الله بكم لاحقون أتاكم ما توعدون اللهم اغفر لأهل بقيع الغرقد

“Amani ya Allaah iwe juu yenu wakazi waumini na waislamu. Nasi – Allaah akitaka – tutaungana na nyinyi. Kimekujieni kile mlichoahidiwa. Ee Allaah! Wasamehe watu wa al-Baqiy´ al-Gharqad.”[3]

Imekuja katika tamko lingine:

نسأل الله لنا ولكم العافية

“Tunamuomba Allaah juu yetu sisi na nyinyi afya.”

Ni lazima kwa muislamu afanye yale yaliyofanywa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi anapoyatembelea makaburi na mfano wa yale aliyowafunza Maswahabah; awatolee salamu, awaombee du´aa ya msamaha na rehema na aseme:

نسأل الله لنا ولكم العافية

“Tunamuomba Allaah juu yetu sisi na nyinyi afya.”

Haya ndio matembezi yanayokubalika katika Shari´ah.

Vivyo hivyo pindi anapolitembelea kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Madiynah. Anapotembelea msikiti kisha akatembelea kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anatakiwa kumtolea salamu, kumwombea du´aa na aseme kumwambia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), jamaa zake na Maswahabah zake:

جزاك الله عن أمتك خيرا

“Allaah akujaze kheri juu ya Ummah wako.”

Vivyo hivyo pindi anapoyatembelea makaburi ya waja wema ambapo anatakiwa kuwaombea msamaha, rehema na amwombe Allaah afya.

Kuhusu kaburi la Yuunus haitambuliki kuwa liko Niynwaa[4]. Makaburi ya Mitume wote hayajulikani wala kutambulika. Madai ya kwamba lipo Niynwaa au kwenginepo ni madai batili yasiyokuwa na msingi wowote.

Wanazuoni wamesema kuwa hakuna kaburi la Mtume yeyote linalotambulika kabisa isipokuwa tu kaburi la Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambalo liko Madiynah. Vinginevyo kaburi la Nabii Ibraahiym liko Hebron katika pango linalotambulika. Hili pekee ndilo linalotambulika. Lakini makaburi ya Mitume wengine waliobaki hayatambuliki; si Yuunus wala Manabii na Mitume wengineo. Makaburi hivi sasa hayatambuliki. Yeyote anayedai kuwa kaburi la Yuunus au Mtume mwengine linatambulika mahali lilipo ni wongo na haina msingi wowote.

Hatumtambui Mtume anayeitwa Jarjaysh na wala haitambuliki kuna miongoni mwa Mitume anayeitwa hivo.

Kinacholengwa ni kwamba hakuna kaburi la Mtume anayetambulika mbali na kaburi la Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambalo lipo Madiynah na kaburi la Nabii Ibraahiym ambalo lipo katika pango inayotambulika. Matembezi haya yanayokubalika katika Shari´ah ni kwa ajili ya wanamme peke yao.

Kuhusu wanawake ni jambo halikuwekwa katika Shari´ah kuyatembelea makaburi kwa mujibu wa maoni sahihi. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewalaani wanawake wenye kuyatembelea makaburi. Kwa hiyo hayo yakafahamisha kuwa haifai kwa wanawake kuyatembelea makaburi. Matembezi yanakuwa kwa wanamme peke yao kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Hayo ni kutokana na zile Hadiyth Swahiyh kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amewalaani wanawake wenye kuyatembelea makaburi. Haya yamekuja katika Hadiyth ya Abu Hurayrah, Hadiyth ya Hassaan bin Thaabit na Hadiyth ya Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhum). Kwa hivyo haikuwekwa katika Shari´ah na wala haijuzu kwao kuyatembelea. Lakini wanawaombea du´aa waislamu waliokufa majumbani mwao, katika misikiti na kila mahali. Wanapotembelea Madiynah basi wanamuombea du´aa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) msikitini au majumbani mwao na wanamswalia na kumtolea salamu popote (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Msilifanye kaburi langu ni lenye kutembelewa mara kwa mara na wala majumba yenu kuwa ni makaburi na niswalieni. Kwani hakika swalah zenu zinanifikia popote mnapokuwa.”[5]

Pindi muumini wa kiume na muumini wa kike atapomswalia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) popote anapokuwa basi inamfikia. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika Allaah anao Malaika wanaozunguka ambao wanafikisha salamu kutoka kwa Ummah wangu.”[6]

Kwa hivo kilichowekwa katika Shari´ah kwako dada muulizaji ni wewe kumswalia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mahali popote na Mitume wengine waliosalia (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam).

Kuhusu kutembelea kaburi hili ambalo inasemekana kuwa ni la Yuunus ni kitu kisichokuwa na msingi. Aidha haifai kwa wanawake kuyatembelea makaburi kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi. Lakini wanawaombea waislamu waliokufa na wanawaombea msamaha waislamu waliokufa popote wanapokuwa.

Kuhusu matembezi ya makaburi ya kizushi ni pale ambapo mtu atayatembelea kwa ajili ya kuswali, kufanya kisomo na kuomba du´aa karibu nayo. Matembezi aina hii ni ya ki-Bid´ah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”[7]

Lakini akiwaomba wale waliyomo ndani ya makaburi, akawataka uokozi au akaomba uombezi kutoka kwao basi hii ndio shirki kubwa ambayo ilikuwa inafanywa na washirikina pambizoni na makaburi. Kwa hiyo ni lazima kutahadhari kutokamana na hayo na kumnasihi anayefanya hivo pamoja na kutubia kwa Allaah kutokamana na hayo.

[1] Muslim (976).

[2] Muslim (974).

[3] Muslim (974).

[4] Tazama https://en.wikipedia.org/wiki/Nineveh_Governorate

[5] Ahmad (8586).

[6] Ahmad (4198) na an-Nasaa´iy (1282).

[7] Muslim (1718).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 28-32
  • Imechapishwa: 07/04/2022