05. Kuyatembelea makaburi ni kwa wanamme tu pasina wanawake

Swali: Je, kuna ubaya wowote wanawake wakitoka kwenda kuyatembelea makaburi wakiambatana na Mahaarim wao? Je, maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):

حَتَّىٰ زُرْتُمُ الْمَقَابِرَ

”Mpaka muingie makaburini.”[1]

yanawahusu wanamme peke yao pasi na wanawake?

Jibu: Matembezi ni maalum kwa wanamme. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewakataza wanawake kuyatembelea makaburi na kuyasindikiza majeneza. Imesihi kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amewalaani wanawake wenye kuyatembelea makaburi. Kwa hivyo haifai kwa wanawake kuyatembelea makaburi na wala kuyasindikiza majeneza kuelekea makaburini. Inafaa kwake kuswali pamoja na watu msikitini, Muswallaa au nyumbani. Hapana vibaya kufanya hivo. Lakini kuyatembelea makaburi au kwenda kwake pamoja na watu makaburini ni kitu kisichojuzu kwake. Haya ndio maoni sahihi zaidi ya wanazuoni.

Kuhusu maneno Yake (Subhaanahu wa Ta´ala):

أَلْهَاكُمُ التَّكَاثُرُ حَتَّىٰ زُرْتُمُ الْمَقَابِرَ

“Kumekushughulisheni kutafuta wingi. Mpaka mwingie makaburini.”[2]

makusudio ni kifo. Kwa msemo mwingine mpaka mtakapopelekwa makaburini hali ya kuwa mmeshakufa. Haihusiani na matembezi yanayotambulika. Kinacholengwa ni kuwatahadharisha watu kujishughulisha na kukusanya mpaka wakafa. Ameita kuwa ni ´matembezi` kwa sababu habaki daima ndani ya kaburi. Ni matembezi. Baada ya hapo atatoka siku ya Qiyaamah ima kuelekea Peponi au kuelekea Motoni.

Makaburi sio kituo cha mwisho. Bali kituo cha mwisho ni ima Peponi au Motoni. Watu wameyatembelea makaburi na watabaki ndani ya makaburi mpaka kufufuliwa na kukusanywa. Itapofika siku ya Qiyaamah watatolewa ndani ya makaburi na Allaah atawafanyia hesabu na kuwalipa juu ya matendo yao. Wenye kumcha Allaah wataingizwa Peponi, makafiri wataingizwa Motoni na wale waislamu waliokuwa wakimuasi Allaah watakuwa khatarini; wanaweza kusamehewa na hivyo wakaingizwa Peponi na pia wanaweza kuadhibiwa kwa kiasi cha madhambi yao kisha baada ya kuadhibiwa kwa vile wanavostahiki Allaah atawatoa nje ya Moto na kuwaingiza Peponi. Haya ni kwa mtazamo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

Kwa kumalizia maneno Yake (Ta´ala):

أَلْهَاكُمُ التَّكَاثُرُ حَتَّىٰ زُرْتُمُ الْمَقَابِرَ

“Kumekughafilisheni kukusanya kwa wingi. Mpaka muingie makaburini.”[3]

kinacholengwa sio yale matembezi yanayotambulika. Hapa kinachokusudiwa ni kifo. Bi maana kumekushughulisheni kukusanya kwa wingi duniani na mmeipupia mpaka mwishowe mmekufa na kupelekwa makaburini. Allaah ameita kuwa ni matembezi kwa sababu hawatobaki ndani ya makaburi milele. Wao ni watembezi na siku ya Qiyaamah watatoka ndani ya makaburi na kuingizwa ima Peponi au Motoni. Hivo ndivo zimefahamisha Aayah tukufu, Hadiyth ambazo ni Swahiyh na waislamu wakaafikiana juu yake. Amesema (Jalla wa ´Alaa) ndani ya Kitabu Chake kitukufu:

زَعَمَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَن لَّن يُبْعَثُوا ۚ قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتُبْعَثُنَّ ثُمَّ لَتُنَبَّؤُنَّ بِمَا عَمِلْتُمْ ۚ وَذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

”Waliokufuru wamedai kwamba hawatofufuliwa kamwe. Sema: “Bali hapana! Naapa kwa Mola wangu! Bila shaka mtafufuliwa, kisha mtajulishwa kwa yale yote mliyoyatenda, na hayo kwa Allaah ni mepesi.”[4]

Allaah atawakusanya watu siku ya Qiyaamah na atawafufua kutoka ndani ya makaburi yao kisha atawalipa kwa matendo yao; yakiwa ni mazuri atawalipa mazuri, na yakiwa ni ya maovu atawalipa uovu.

Kwa hivyo ni lazima kwa kila muislamu wa kiume na wa kike kujiandaa kwa ajili ya siku hii na kupupia juu ya matendo mema ili apate furaha  na afuze kuokoka siku ya Qiyaamah. Hili ni jambo la lazima kwa kila ambaye ´ibaadah ni zenye kumuwajibikia ardhini miongoni mwa majini na watu. Ni lazima kwa kila ambaye ´ibaadah ni zenye kumuwajibikia miongoni mwa waarabu na wasiokuwa waarabu, watu na majini, makafiri na waislamu, wajiandae kwa ajili ya siku hii. Makafiri waingie ndani ya Uislamu na wanyooke juu yake ili wapate ukombozi siku ya Qiyaamah.

[1] 102:02

[2] 102:01-02

[3] 102:01-02

[4] 64:07

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 25-27
  • Imechapishwa: 07/04/2022