03. Kuihakikisha taqwa


Lengo la tatu: Kuihakikisha taqwa

Miongoni mwa malengo ya hajj ni kumcha Allaah (Jalla wa ´Alaa). Hakika Allaah ameusia kwa wingi katika Aayah za hajj, pamoja na uchache wake, juu ya kumcha. Kwa kuwa kunapatikana katika hajj sababu zinazopelekea katika kumcha Allaah jambo ambalo halipatikani katika jambo lingine. Hili ni pamoja na kuwa na ufahamu wa kisawasawa juu ya uhakika wa hajj na malengo yake. Wasia wa kumcha Allaah (´Azza wa Jall) umekariri katika mtiririko wa Aayah za hajj katika Suurah “al-Baqarah”. Allaah (Ta´ala) amesema katika Aayah ya kwanza miongoni mwa Aayah hizi:

وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ

“Mcheni Allaah na tambueni ya kwamba Allaah ni mkali wa kuadhibu.”[1]

Katika Aayah ya pili miongoni mwa Aayah hizi amesema (Subhaanah):

وَتَزَوَّدُوا فَإِنَّ خَيْرَ الزَّادِ التَّقْوَىٰ

“Chukueni masurufu. Na hakika bora ya masurufu nikumcha Allaah.”[2]

Allaah (Subhaanah) amekhitimisha Aayah ya hajj kwa kusema:

وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَاعْلَمُوا أَنَّكُمْ إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ

”Mcheni Allaah na tambueni ya kwamba Kwake mtakusanywa.”[3]

Amesema (Subhaanah) katika Suurah “al-Hajj”:

ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّـهِ فَإِنَّهَا مِن تَقْوَى الْقُلُوبِ

“Ndivyo hivyo na yeyote anayeadhimisha ´ibaadah za Allaah, basi hayo ni katika uchaji wa nyoyo.”[4]

لَن يَنَالَ اللَّـهَ لُحُومُهَا وَلَا دِمَاؤُهَا وَلَـٰكِن يَنَالُهُ التَّقْوَىٰ مِنكُمْ

”Haimfikii Allaah nyama zake wala damu yake, lakini unamfikia uchaji kutoka kwenu.”[5]

Kumcha Allaah ndio wasia mkubwa na akiba bora kabisa juu ya siku ya Qiyaamah. Ndio wasia wa Allaah (Subhaanah) juu ya viumbe Wake wa mwanzo na wa mwisho. Amesema (Subhaanah):

وَلَقَدْ وَصَّيْنَا الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِن قَبْلِكُمْ وَإِيَّاكُمْ أَنِ اتَّقُوا اللَّـهَ

”Hakika Tumewausia wale waliopewa Kitabu kabla yenu na nanyi [pia tunakuusieni] kwamba: “Mcheni Allaah.”[6]

Vilevile ndio wasia wa Mtume mtukufu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya Ummah Wake. Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapomtuma kiongozi wa jeshi basi kwanza anaanza kumuuasia yeye mwenyewe kumcha Allaah juu ya nafsi yake na amche Allaah vilevile juu ya wale waumini walio pamoja naye. Mara nyingi alikuwa akiusia katika Khutbah zake. Pindi alipowatolea watu Khutbah katika hajj ya kuaga siku ya Nahr aliwausia watu juu ya kumcha Allaah (´Azza wa Jall). Wema waliotangulia (as-Salaf as-Swaalih) walikuwa ni wenye kuendelea kuusiana juu ya kumcha Allaah. Hilo si kwa jengine isipokuwa ni kwa sababu ndio akiba bora zaidi ambayo inamfikisha mtu katika radhi za Allaah (´Azza wa Jall). Wakati mtu mmoja alipomwambia ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh):

“Mche Allaah!”

´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) akamjibu kwa kumwambia:

“Hakuna kheri kwenu msipotwambia hivo. Wala hakuna kheri kwetu tusipoyakubali hayo.” Kuna nukuu nyingi kutoka kwa Salaf juu ya haya.”

Ni uzuri ulioje muhujaji kutoka katika hajj yao wakiwa wamejichukulia zawadi ya akiba hii tukufu na iliobarikiwa. Hakika wasia wa Allaah (´Azza wa Jall) juu ya kumcha Allaah uliotajwa mara nyingi katika Aayah za hajj na kuita Kwake (Subhaanah) kuwaita wale wenye akili kwamba wamche, ni dalili inayofahamisha ya kwamba wale wenye akili na busara – ambao Allaah amewakirimu kuweza kuhiji – wanatakiwa kufanya jambo hilo liwe ni miongoni mwa malengo yao makubwa kabisa katika kuhiji kwao. Wanatakiwa pia kuzitumia akili zao na busara zao katika nembo hizo tukufu waweze kufaidika kumcha Allaah. Hajj ni masomo makubwa juu ya kumcha Allaah na ni mlango mkubwa miongoni mwa milango yake. Zile nembo zake zinazingatiwa ni msaada mkubwa kabisa kwa mtu kuhakikisha kumcha Allaah (´Azza wa Jall). Hilo ni kwa sababu katika matendo ya hajj kuna mazoezi ya nafsi juu ya kulazimiana na kumcha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na kuelekea kumuabudu na wakati huohuo mja kujiepusha na hali ambayo alikuwa nayo hapo kabla katika kukwepa mambo fulani na kutoshikamana na maamrisho ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).

[1] 02:196

[2] 02:197

[3] 02:203

[4] 22:32

[5] 22:37

[6] 04:131

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Maqaaswid-ul-Hajj, uk. 16-18
  • Imechapishwa: 12/08/2018