02. Kufuzu kwa kupata radhi za Allaah na kuokoka kutokamana na Moto

Lengo la pili: Kupata radhi za Allaah (Tabaaraka wa Ta´ala)

Miongoni mwa malengo ya hajj ni kufuzu kwa kupata radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), kuokoka kutokamana na Moto, kufuzu kwa kupata msamaha na huruma Wake (Subhaahahu wa Ta´ala). Kuna dalili nyingi zinazofahamisha juu ya malengo haya makubwa. Miongoni mwayo ni pamoja na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ambaye atahiji kwa ajili ya Allaah na asizungumze maneno ya kipuuzi wala asifanye tendo la ndoa na wala asifanye madhambi, basi anarejea kama siku ambayo alimzaa mama yake.”[1]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hajj yenye kukubaliwa haina malipo isipokuwa Pepo.”[2]

Amesema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale alipokuwa akimwambia ´Amr bin al-´Aasw:

“Je, hujui ya kwamba Uislamu unafuta yale yaliyokuwa kabla yake, kwamba kuhajiri kunafuta yale yaliyokuwa kabla yake na kwamba hajj inafuta yale yaliyokuwa kabla yake?”[3]

Pia amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Fuatisheni kati ya Hajj na ´Umrah. Kwani viwili hivyo ni vyenye kuondosha ufakiri na dhambi kama ambavyo kile chombo cha kufua chuma kinavyoondoa uchafu wa dhahabu na fedha. Hajj yenye kukubaliwa haina malipo isipokuwa Pepo.”[4]

Kufuzu kwa kupata radhi za Allaah (´Azza wa Jall) ndio neema kubwa na tukufu zaidi. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللَّـهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ وَعَدَ اللَّـهُ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا وَمَسَاكِنَ طَيِّبَةً فِي جَنَّاتِ عَدْنٍ ۚوَرِضْوَانٌ مِّنَ اللَّـهِ أَكْبَرُ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Waumini wanaume na waumini wanawake ni marafiki wao kwa wao; wanaamrisha mema na wanakataza maovu na wanasimamisha swalah na wanatoa zakaah na wanamtii Allaah na Mtume Wake – hao Allaah atawarehemu. Kwani hakika Allaah ni Mwenye nguvu kabisa, Mwenye hekima. Allaah amewaahidi waumini wanaume na waumini wanawake mabustani yapitayo chini yake mito ni wenye kudumu humo milele na makazi mazuri katika mabustani ya kudumu milele – na radhi kutoka kwa Allaah ndio kubwa zaidi. Huko ndiko kufuzu kukubwa.”[5]

Ametaja (Jalla wa ´Alaa) matendo yao ya mwanzo katika kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kusimamisha faradhi za Uislamu, mambo ya wajibu ya dini, kutendea kazi dini ya Allaah kwa ajili ya kuwatakia kheri waja Wake hali ya kuamrisha mema na kukataza maovu. Halafu akafuatishia hilo (Jalla Sha´nuh) kwa kutaja yale aliyowaandalia hatua kwa hatua ambapo (Subhaanahu wa Ta´ala) akaanza kutaja kwamba amewaandalia mabustani yapitayo chini yake mito, kisha akafuatisha kutaja makazi matukufu na maghorofa ya juu kabisa ambayo amewaandalia wao na nyumba katika mabustani hayo. Halafu baada ya yote hayo akataja karama na neema iliokubwa kabisa; nayo si nyingine ni kule Yeye kuwa radhi nao. Amesema:

وَرِضْوَانٌ مِّنَ اللَّـهِ أَكْبَرُ

“… na radhi kutoka kwa Allaah ndio kubwa zaidi.”

Kisha akamalizia mtiririko wa maneno kwa kusema:

ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Huko ndiko kufuzu kukubwa.”

Radhi za Allaah ndio jambo kubwa kuliko kila neema. Ndio jambo kubwa kuliko Pepo na kubwa kuliko kila neema Peponi. Kwani ndio karama kubwa na zawadi tukufu zaidi.

Maana hii katika Aayah inawekwa wazi zaidi – japokuwa tayari iko wazi – na yale aliyopokea al-Bukhaariy na Muslim katika “as-Swahiyh” zao kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) atawaambia watu wa Peponi: “Enyi watu wa Peponi!” Waseme: “Tumekuitikia, ee Mola wetu, na tunataka saada Yako.” Je, mmeridhika?” Waseme: “Ni kwa nini tusiridhike ilihali Umetupa yale ambayo Hujampa yeyote katika viumbe Wako.” Ndipo aseme: “Mimi Nakupeni bora kuliko hayo.” Waseme: “Ee Mola wetu! Na ni kitu gani bora kuliko haya?” Aseme: “Nimekuhalalishieni radhi Zangu na kamwe sintokukasirikieni baada yake.”[6]

al-Haakim amepokea katika “al-Mustadrak” yake kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kupitia kwa Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu wa Peponi watapoingia Peponi Allaah (´Azza wa Jall) atasema: “Je, mnatamani kitu niwazidishieni?” Waseme: “Ee Mola wetu! Ni kipi cha ziada juu ya yale Uliyotupa?” Akasema: “Radhi Zangu ni kubwa zaidi.”[7]

Bi maana ni kubwa zaidi kuliko Pepo na yaliyomo ndani yake.

Kila muislamu anatakiwa kuliweka lengo hili mbele ya macho yake, alihudhurishe moyoni mwake, atafute katika hajj yake pindi anapoenda katika Nyumba ya Allaah Tukufu kupata radhi za Allaah (Tabaarak wa Ta´ala), msamaha Wake na kuachiwa huru kutokamana na Moto. Vilevile apupie katika kulihudhurisha lengo hili akilini mwake katika kila mahali, kila anaposimama na katika kila hali – ni mamoja katika hajj na kwenginepo. Kwa sababu Aayah hii ikikita kwenye moyo na yakawa yale yaliyofahamishwa nayo ndio malengo ya mtu, basi hali zake zote zitatengemaa na mambo yake yote yatakuwa mazuri.

[1] al-Bukhaariy (1521) na Muslim (1350).

[2] al-Bukhaariy (1773) na Muslim (1349).

[3] Muslim (121).

[4] at-Tirmidhiy (810) na an-Nasaa´iy (2631) kupitia kwa Ibn Mas´uud kwa (Radhiya Allaahu ´anh) kwa cheni ya wapokezi ilio nzuri (Hasan).

[5] 09:71-72

[6] al-Bukhaariy (6549) na Muslim (2829).

[7] al-Haakim katika ”al-Mustadrak” (01/146) ambaye amesema: ”Ni Swahiyh kwa mujibu wa masharti ya al-Bukhaariy na Muslim na hawakuipokea.” adh-Dhahabiy ameafikiana naye na inatolewa ushahidi na ilio kabla yake.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Maqaaswid-ul-Hajj, uk. 11-15
  • Imechapishwa: 12/08/2018