Wazazi hawataki asuhubiane na marafiki wazuri

Swali: Mimi namshukuru Allaah kuona kwamba Allaah ameniongoza katika haki, lakini ninapata ugumu nyumbani na kwamba familia yangu wananiamuru niwaache ndugu zangu kwa ajili ya Allaah, wanasema hawa ni kama kundi lililopotoka, wananizuia kufanya mema na kunizuia kuswali swalah ambazo wakati mwingine baada yake kuna kikao cha kusoma kitabu au mfano wake. Pia hawanisikilizi kwa sababu mimi ni mwenye juhudi na wananichukulia kama mtoto na wananizuia kusikiliza kanda za dini na wakisema hizi ni za upotovu na mfano wa hayo.

Jibu: Kwa hali yoyote ni juu yako, ee mwanangu, kufanya juhudi kadiri uwezavyo kuwafurahisha wazazi wako, kuzingatia hisia zao, pamoja na familia yako kwa maneno mazuri na mtindo mwema. Lakini si juu yako kuwatii katika jambo linalokudhuru au katika kumuasi Mola wako, kama ilivyotangulia. Nenda kutafuta elimu na nenda kuswali swalah ya mkusanyiko, lakini kwa mtindo mzuri na maneno mazuri. Aidha sikiliza kanda nzuri na uwahimize – wazazi wako, ndugu zako na jamaa zako – kusikiliza yale yanayowanufaisha kwa maneno mazuri na mtindo mwema, si kwa ukali, kwa nguvu na wala kujiona juu yao. Bali uwe na maneno mazuri na mtindo mwema ili uepuke ghadhabu za wazazi wako na pia uweze kutekeleza yale ambayo Allaah amekuwajibishia.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3279/حكم-منع-الاباء-ابناءهم-من-مصاحبة-الاخيار
  • Imechapishwa: 07/08/2026