Swali: Mara nyingi katika mabaraza ya wanawake tunawaona wavulana na wasichana wadogo chini ya miaka saba na mfano wa hivo wakivaa mavazi mafupi, yenye kubana, mitindo ya ajabu ya nywele, mitindo ya nywele ya wasichana wadogo inayofanana  na mitindo ya nywele ya wavulana. Tunapoongea na mama zao na kuwanasihi wanatumia hoja kwamba bado ni wadogo. Tunaomba utubainishe vya kutosha kuhusu qadhiya ya mavazi ya watoto na kukata vichwa vyao.

Jibu: Ni jambo linalojulikana kwamba mtu huathirika kwa kitu tangu utotoni mwake na anabaki katika hali hiyo baada ya kukuwa. Kwa ajili hii ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha mtoto aamrishwe kuswali pale anapokuwa na miaka saba na kuwapiga kwa ajili yake wanapofikisha miaka kumi. Yote haya ili azowee. Mtoto anakuwa juu ya yale aliyozowea. Msichana mdogo akizowea kuvaa mavazi mafupi yanayofika mpaka kwenye magoti na mavazi mafupi yanayofika mpaka kwenye visugudi au kwenye mabega, basi haya itamwondoka na atazowea mavazi haya baada ya kukuwa kwake.

Kadhalika inapokuja katika nywele. Mwanamke anatakiwa kuwa na nywele zinazotofautiana na nywele za wanaume. Akiwa na nywele kam za wanaume, basi amejifananisha nao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemlaani mwanamke mwenye kujifananisha na wanaume. Itambulike kuwa familia wataulizwa juu ya watoto hawa, juu ya kuelekezwa kwao na kuwalea kwao. Kama alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwanaume ni mchungi juu ya watu wa nyumbani kwake na ataulizwa juu ya kile alichokichunga.”

Tahadharini juu ya kuzembea. Mtu anatakiwa awe makini katika kuwaelekeza watoto wake wa kiume na wa kike na awe na pupa juu yao mpaka Allaah (Tabaarak  wa Ta´ala) aweze kuwarekebisha na wawe ni kipumbazo chake cha macho.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (66) http://binothaimeen.net/content/1479
  • Imechapishwa: 27/01/2020