Mmeniuliza hukumu ya wanawake kutembelea kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baadhi ya wanazuoni wanaona kuwa halina ubaya. Haina maana kwamba kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) lina vigezo vinavyotofautiana na makaburi mengine – sivyo hivo – bali ni kwa sababu kaburi lake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) limezungushwa kwa njia ambayo haiwezekani kulifikia. Kwa msemo mwingine ni kwamba haliwezi kutembelewa. Hata hivo bora ni kuwazuia wanawake kutembelea kaburi lake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa sababu matembezi hayo hayakuwekwa katika Shari´ah, isipokuwa ni matembezi ya kiada. Ni kama ambavo wakienda katika makaburi ya al-Baqiy´; basi wanatakiwa kuzuiwa kuingia ndani.

Pengine mtu akasema kuwa kule kusimama kwao nje ya kuta za makaburi ya al-Baqiy´ hakuitwi kuwa ni matembezi. Kwa hiyo waachwe waende, lakini lakini bora na lililo salama zaidi ni kuepuka kufanya hivo. Endapo mwanamke anataka kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au kuwaombea du´aa wafu, basi anaweza kufanya hivo akiwa nyumbani kwake. Bora kwa wanawake ni wao kubakia majumbani mwao.

Umeulizia pia juu ya Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa):

“Jibriyl alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Hakika Mola wako anakwamrisha kuwaendea watu wa al-Baqiy´ uwaombee msamaha.” Nikasema: “Niwaambie nini, ee Mtume wa Allaah?” Sema:

السَّلامُ عَلَيْكُمْ أَهْلَ الدِّيَارِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُسْلِمِين,و يرحم الله المستقدمين منا و المستأخرين,وَإِنَّا إِنْ شَاءَ اللهُ بكم لاحِقُونَ نَسْأَلُ الله لَنَا وَلَكُمْ الْعَافِية

“Amani ishuke juu yenu, watu wa nyumba za waumini na waislamu. Allaah awarehemu wale waliotangulia katika sisi na wanaokuja nyuma. Na sisi – atakapo Allaah – tutakutana na nyinyi. Namuomba Allaah atupe sisi na nyinyi afya njema.”[1]

Kama unavojionea mwenyewe Hadiyth haisema chochote wazi kuhusu matembezi na kwa ajili hiyo haitakiwi kuikinzanisha na Hadiyth ambazo waziwazi zinaharamisha wanawake kuyatembelea makaburi. Hata hivyo hapana shaka juu ya kufaa kwa mwanamke ambaye imetokea akayapitia makaburi pasi na kukusudia kuyatembelea na hivyo akawatolea salamu. Namna hiyo ndivo inavotakiwa kufahamika Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) na makatazo yatabaki vilevile. Kwa ajili hiyo hitimisho la mtunzi wa “al-Mishkaat” si zuri. Kwa vile Hadiyth haikusema waziwazi basi haitakiwi kuthibitisha wala kukata chochote.

Isitoshe mwanamke kuyatembelea makaburi wanazuoni wametofautiana juu ya maoni matatu:

1- Kufaa. Miongoni mwa dalili zao ni Hadiyth hii. Wamedai kuwa Hadiyth zinazokataza zimefutwa.

2- Imechukizwa. Dalili yao ni Hadiyth ya Umm ´Atwiyyah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesema:

“Tumekatazwa kusindikiza jeneza licha ya kuwa hatukufanyiwa mkazo.”[2]

3- Uharamu. Dalili yao ni maneno yake Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhuma) aliyesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewalaani wanawake wenye kuyatembelea makaburi, wenye kuyafanya ni mahali pa kuswalia na wenye kuyatia mataa.”[3]

 Wanasema kuwa Hadiyth ambazo wamejengea kwazo hoja wale wenye kuonelea kuwa inafaa hazisemi wazi kufaa kwa mwanamke kuyatembelea makaburi mpaka iweze kusemwa kuwa zinakinzana na Hadiyth zinazokataza. Iwapo mtu atakadiria kuwa zimesema wazi, basi itambulike kuwa Hadiyth zinazokataza ndio  salama zaidi kufuatwa. Kwa sababu hizo zinajulisha juu ya uharamu wa matembezo na hizo za upande wa pili zinajulisha juu ya kufaa. Kujiepusha na haramu kuna haki zaidi kuliko kufanya kilichopendekezwa. Madai ya kusema kwamba zimefutwa ni yenye kutupiliwa mbali kwa sababu kwa sababu miongoni mwa sharti za kufutwa ni lazima itambulike tarehe ya kile chenye kufuta. Hakuna dalili yoyote inayofahamisha kuwa Hadiyth zinazojuzisha zimekuja baada ya makatazo. Aidha madai hayohayo yanaweza kutumiwa na wale wanaosema kuwa ni haramu na hivyo wakasema kuwa Hadiyth za kujuzisha zilikuja kabla ya Hadiyth za makatazo na hivyo imezifuta. Maoni yanayoharamisha ni yenye nguvu zaidi upande wa dalili na sababu. Wanawake kuyatembelea makaburi kunaweza kupelekea katika shari na uharibifu kitu ambacho baadaye kikapelekea kuwakataza hata kama kusingelikuweko dalili zinazoharamisha. Kusemwe nini ilihali Hadiyth zinawalaani wanawake wenye kuyatembelea makaburi?

[1] Muslim (974).

[2] al-Bukhaariy (1278) na Muslim (938).

[3] Abu Daawuud (3236), at-Tirmidhiy (320), an-Nasaa’iy (2043) na Ahmad (2030). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Silsilat-ul-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah” (225).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/325-327)
  • Imechapishwa: 14/06/2021