Wanataka kutumia ardhi ambayo walizika ndani yake watu watatu

Swali: Mtu ana shamba la kilimo ambapo akazikwa humo mmoja wa watoto wake, kisha akafa mtoto mwingine akamzika pamoja na ndugu yake katika kaburi hilohilo, kisha baadaye akahamisha mifupa ya mke wake na kumweka katika kaburi hilohilo kwa sababu kaburi lake lilipitiwa na barabara. Hivyo kaburi hilo likawa na watu watatu. Baada ya baba kufariki na watoto wake kukua, wanataka kujenga katika ardhi hiyo lakini kaburi liko katikati na linawaletea usumbufu. Je, inajuzu kuhamisha mabaki ya mifupa kutoka kaburi hilo kwenda makaburi ya waislamu ili waweze kuitumia ardhi hiyo?

Jibu: Hili ni kosa kuwazika wote katika ardhi hiyo. Bali lililowajibika ni kumzika kila mmoja katika kaburi lake peke yake ikiwa inawezekana na wawe katika makaburi ya waislamu, si katika ardhi yao, wala nyumbani kwao, wala kwenye uzio wao. Wajibu ni wawe pamoja na waislamu katika makaburi ya waislamu.

Hivyo watoto waliopo wanapaswa kuhamisha mifupa kwenda makaburi ya ummah. Kila mifupa iwe katika kaburi lake peke yake, katika shimo lake peke yake na uso wake usawazishwe kama kaburi ili liheshimiwe kama makaburi mengine lisikanyagwe wala kudhalilishwa. Wajitahidi kuweka mifupa ya wa kwanza peke yake, ya wa pili peke yake na ya wa tatu peke yake; kila mmoja katika shimo lake. Kisha wasawazishe juu yake kama ilivyo makaburi katika makaburi ya waislamu yaliyo karibu nao. Hakuna ubaya kuitumia ardhi hiyo baada ya hapo.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3373/حكم-نبش-رفات-موتى-دفنوا-في-قبر-واحد
  • Imechapishwa: 20/08/2026