Swali: Ni lazima kwa mzee aliyepoteza fahamu, mtu  mwenye ugonjwa wa akili, mtoto na mwendawazimu kufunga?

Jibu: Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amewawajibishia tu wale watu wenye uwezo wa kufanya ´ibaadah. Bi maana wawe ni wenye akili ya kuweza kuyafahamu mambo. Ama wale wasiokuwa na akili ´ibaadah haiwalazimu. Kujengea juu ya haya funga haimlazimu mwendawazimu. Wala haimlazimu mdogo ambaye hajakuwa na uwezo wa kupambanua mambo. Hii ni rehema ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Vivyo hivyo inahusiana na mwenye ugonjwa wa akili ambaye ni kama mwendawazimu. Kadhalika mzee sana kiasi cha kwamba ameondokwa na fahamu. Mtu kama huyu haimlazimu kufunga, kuswali wala kujisafisha, kwa sababu mzee aliyepoteza fahamu ni kama mtoto mdogo ambaye hajakuwa na uwezo wa kupambanua mambo.

Hata hivyo bado wanawajibika kutekeleza mambo ya wajibu ya kipesa. Wasimamizi wao wanatakiwa kuwatolea zakaah za mali zao kwa sababu zakaah imefungamana na pesa. Allaah (Ta´ala) amesema:

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا

“Chukua katika mali zao zakaah uwatakase na ziwazidishie kwazo.”[1]

Amesema “chukua katika mali zao zakaah” na hakusema “Wachukue”. Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia Mu´aadh (Radhiya Allaahu ´anh) pindi alipomwagiza kwenda Yemen:

“Wajuze kwamba Allaah amefaradhisha juu yao zakaah ambayo inatakiwa kuchukuliwa kutoka kwa matajiri wao na wapewe mafukara wao.”[2]

Amebainisha kuwa zakaah inatakiwa kuchukuliwa kutoka katika mali zao hata kama ni yenye kuchukuliwa kutoka kwa mmiliki. Uwajibu wa kimali hauanguki kutoka kwa mtu mwenye hali kama hii. ´Ibaadah za kimwili, kama mfano wa swalah na swawm, ndivyo vyenye kuanguka kwa watu kama hawa kwani hawana akili.

Ama ambaye ameondokwa na akili/kuzimia kwa sababu ya maradhi, wanachuoni wengi wanaona kuwa haimlazimu kuswali. Mgonjwa akitokwa na akili/akizimia kwa muda wa siku moja au siku mbili, haimlazimu kulipa, kwa sababu hana akili. Mtu kama huyu hana hukumu moja kama aliyelala ambaye Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu yake:

“Kalamu imenyanyuliwa kwa watu aina tatu; aliyelala mpaka anapoamka, mtoto mpaka anapobaleghe na mwendawazimu mpaka anapopata akili.”[3]

Kwani mwenye kulala ana uwezo wa kuyadiriki mambo kwa njia ya kwamba anaweza kuamka endapo ataamshwa. Hivo ni tofauti na aliyeondokwa na akili/aliyezimia. Hapa ni pale ambapo si yeye ndiye kasababisha kuondokwa na akili/kuzimia. Ama ikiwa yeye ndiye kasababisha kuodokwa na akili/kuzimia (kama mfano wa kutumia dawa za usingizi) basi atalazimika kulipa swalah zilizompita.

[1] 09:103

[2] al-Bukhaariy (1395) na Muslim (19).

[3] Abu Daawuud (4405) na Ahmad (1362). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa’” (2/5).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (19/85-87)
  • Imechapishwa: 23/05/2019