Wameswali Maghrib kabla ya ´Aswr kwa kusahau

Swali: Jopo la watu wamesahau kuswali ´Aswr na hawakukumbuka isipokuwa wakati waliposikia kunaadhiniwa Maghrib. Wakaanza kuswali Maghrib kisha baadaye ´Aswr. Ni ipi hukumu?

Jibu: Mtu akisahau swalah au usingizi ukamchukua na asiwe na mtu wa kumuamsha au kumkumbusha mpaka ukatoka wakati wake, mambo ni kama alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule mwenye kupitikiwa na usingizi au akaisahau swalah, basi aiswali pale atapoikumbuka. Haina kafara nyingine isipokuwa hiyo.”[1]

Katika hali kama hii ya muulizaji anatakiwa kwanza kuswali ´Aswr kisha Maghrib, ili mpangilio iwe vile alivyofaradhisha Allaah (´Azza wa Jall). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipopitwa na swalah kadhaa katika vita vya Khandaq alizilipa kwa mpangilio. Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayi wa sallam) amesema:

 “Swalini kama mlivyoniona nikiswali.”[2]

Wakati mlipokuja msikitini na mkawakuta watu wanaswali Maghrib, mngejiunga nao kwa nia ya ´Aswr. Kisha wakati imamu atakapomaliza kuswali Maghrib, mkakamilisha swalah yenu la ´Aswr. Hivyo mkawa mmeswali Maghrib kwa mkusanyiko na ´Aswr kivyenu. Kutofautiana kwa nia ya imamu na maamuma haidhuru. Kwa sababu matendo ni yaleyale. Alichokataza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kutofautiana na imamu kimatendo na si kinia. Kwa mle mlifanya kwa ujinga ambapo mlianza kuswali Maghrib kabla ya ´Aswr, haina neno juu ya jambo hilo.

[1] al-Bukhaariy (597) na Muslim (684).

[2] al-Bukhaariy (631).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/223)
  • Imechapishwa: 15/04/2026