Wameswali ´Ishaa kwa kufupisha kwa sababu ya mvua

Swali: Mtu aliswali kwa mkusanyiko swalah ya Maghrib wakati wa mvua, kisha akajumuisha ´Ishaa pamoja na Maghrib, lakini akaswali ´Ishaa kwa kuipunguza, kwa sababu ya kutokujua namna ya kukusanya swalah. Baada ya siku nikajua jambo hili, nikawaambia warudie swalah yao. Je, nimekosea kwa kufanya hivyo?

Jibu: Umefanya sahihi. Kupunguza swalah ni kwa msafiri peke yake. Ama mgonjwa au anayejumuisha swalah akiwa katika hali ya wenyeji, haifai kupunguza swalah. Baadhi ya watu wa kawaida huita kukusanya swalah kwamba ni kufupisha swalah, lakini hii si sahihi. Kufupisha ni kuswali swalah ya Rak´ah nne kuwa Rak´ah mbili. Hii huitwa kupunguza. Ama kujumuisha Dhuhr na ´Aswr, Maghrib na ´Ishaa, hii huitwa kukusanya na si kufupisha. Kukusanya ´Aswr na Dhuhr kutokana na mvua au ugonjwa, kukusanya Maghrib na ´Ishaa kutokana na mvua, safari au ugonjwa, hii yote huitwa kukusanya na si kufupisha.

Ikiwa mtu amejumuisha kwa sababu ya ugonjwa au mvua, basi anaswali Dhuhr Rak´ah nne, ´Aswr Rak´ah nne na ´Ishaa Rak´ah nne. Haswali Rak´ah mbilimbili. Rak´ah mbili ni kwa msafiri tu, katika safari peke yake. Hatufahamu kuwa kuna anayeswali Rak´ah mbili isipokuwa msafiri akiwa safarini. Ama mgonjwa aliyeko mjini, wakati wa mvua au wakati wa utelezi wa ardhi, yeye huswali Rak´ah nne. Akijumuisha Maghrib na ´Ishaa, basi ataswali Maghrib Rak´ah tatu na ´Ishaa Rak´ah nne. Hili ni kwa maafikiano ya wanazuoni, hakuna makinzano katika hilo. Waislamu wameafikiana kwamba swalah ya mtu aliye katika hali ya ukazi ni Rak´ah nne, hata ikiwa ni wakati wa mvua au ugonjwa. Dhuhr, ´Aswr na ´Ishaa huswaliwa Rak´ah nne. Fajr hubaki Rak´ah mbili na Maghrib hubaki Rak´ah tatu, katika kila hali; safari na wenyweji.

Kwa hiyo wale walioswali ´Ishaa Rak´ah mbili kwa sababu ya mvua, hali ya kuwa wako mjini na wenyeji, hao wamekosea kosa kubwa kwa maafikiano ya waislamu. Hivyo wanalazimika kurudia swalah ya ´Ishaa. Wakikumbushwa mara moja wakiwa bado hawajatengana, wanakamilisha papohapo na inatosha. Lakini ikiwa muda umetengana na hawakujua isipokuwa baada ya muda mrefu, basi warudie swalah. Imamu na wanaoswali nyuma yake wote warudie swalah.

Swali: Je, warudie kwa mkusanyiko?

Jibu: Ikiwezekana kwa mkusanyiko, hiyo ni bora zaidi. Vinginevyo kila mmoja arudie swalah yake nyumbani.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/2176/حكم-قصر-العشاء-بنية-الجمع-مع-المغرب-وقت-المطر
  • Imechapishwa: 18/07/2026