Vipi vijana wataachana na punyeto?

Swali: Kuna utatuzi wowote wa kiimani na kimatendo mimi kuweza kuachana na kujichua sehemu ya siri kwa sababu mimi nimepewa mtihani wa jambo hilo na hunisumbua mpaka mwezi wa Ramadhaan?

Jibu: Tunamuombea kwa Allaah amponye. Kuhusu utatuzi wa kiimani ni maneno Yake (Tabaarak wa Ta´ala) pale alipowasifu waumini kwa kusema:

وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ إِلَّا عَلَىٰ أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ فَمَنِ ابْتَغَىٰ وَرَاءَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْعَادُونَ

”Na wale ambao wanazihifadhi tupu zao, isipokuwa kwa wake zao au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, basi hao si wenye kulaumiwa. Basi yeyote yule atakayetaka kinyume ya hivo, basi hao ndio wavukao mipaka.”[1]

 Kujichua sehemu ya siri, kwa msemo mwingne punyeto, ni kinyume na wake na wale ambao wamemilikiwa na mikono ya kuume ambao ni wale mateka:

و فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْعَادُونَ

“Basi yeyote yule atakayetaka kinyume ya hivo, basi hao ndio wavukao mipaka.”

Allaah ameeleza kwamba ni kuchupa mpaka. Mtu akishajua kuwa kufanya hivo ni kuvuka mpaka basi hatofanya hivo.

Ama upande wa matishio ya kimwili, basi awaulize madaktari ili abainikiwe kwamba ni miongoni mwa mambo yanayodhuru mwili. Hata kama mtu anahisi raha, lakini ni raha ndogo iliyoambatana na maradhi makubwa. Wako baadhi ya watu walionambia kwamba walipewa mtihani wa jambo hili na matokeo yake wakapewa mtihani wa wasiwasi wa ki-Shaytwaan na dhiki ya kinafsi. Hili ni jambo ambalo haliko mbali. Allaah ni Mwingi wa hekima na amejaalia tone hili liwekwe sehemu maalum:

نِسَاؤُكُمْ حَرْثٌ لَّكُمْ فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أَنَّىٰ شِئْتُمْ

“Wake zenu ni konde kwenu. Hivyo ziendeeni konde zenu vyovyote mpendavyo.”[2]

Mtu anatakiwa kufanya na kuvuta subira. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametaja dawa yenye mafanikio ambayo ni:

“Enyi kongamano la barobaro! Yule atakayeweza miongoni mwenu kuoa basi na aoe. Hakika hilo linamfanya ainamishe macho na inahifadhi utupu wake. Yule asiyeweza basi ni juu yake afunge. Kwani kwake ni kinga.”[3]

[1] 70:31

[2] 02:223

[3] al-Bukhaariy (1905), Muslim (1400), at-Tirmidhiy (1081) na wengineo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (61) http://binothaimeen.net/content/1385
  • Imechapishwa: 24/06/2020