Swali: Baadhi ya nyakati wakati ambapo imamu moja kwa moja anaunganisha kusoma al-Faatihah basi maamuma nao wanaendelea kusoma al-Faatihah. Pamoja na kwamba anajua kuwa waswaliji wanasoma al-Faatihah baada yake, ni vyema akawaachia nafasi nao waweze kufanya hivo na kutendea kazi Sunnah?

Jibu: Hapana shaka kwamba inatakiwa kutendea kazi Sunnah. Hatakiwi kujali kwa ajili ya Allaah lawama za wenye kulaumu. Vinginevyo itawezekanaje kueneza Sunnah ikiwa mtu anawafuata kichwa mchunga watu katika desturi, mazowea na mirengo yao? Lakini yule ambaye anataka kueneza Sunnah basi anatakiwa kuhakikisha kwanza ameitengenezea njia. Kwa msemo mwingine ni kwamba asiwashtukize watu kwayo. Yule ambaye anataka kutokomeza ada hii ambayo hufanywa na maimamu wengi wa misikiti katika nchi hii na kunyamaza kitambo kidogo baada ya kumaliza kwao kusoma al-Faatihah katika swalah za kusoma kwa sauti ya juu, basi anapaswa kujua kuwa si jambo jepesi. Kwa hivyo ni lazima awakumbushe watu juu ya Sunnah Swahiyh juu ya masuala hayo na kwamba kinyamazo hichi kirefu kinachofanywa na baadhi ya maimamu hakina msingi katika Sunnah Swahiyh. Ni lazima awakumbushe maudhui hayo. Hapo ndipo utenda kazi wake wa Sunnah hiyo utakubaliwa na hao watu. Ama kuwashtukiza tu na asinyamaze kitambo kidogo ilihali hapo kabla hakutangulia japo mara moja kuwakumbusha ni jambo gumu kabisa. Ni jambo ambalo linaweza kusababisha vurugu katika baadhi ya misikiti.

Kwa ajili hiyo ni lazima kukusanya kati ya kulingania katika Sunnah na kuitendea kazi. Yote mawili yanahitajika. Huwezi kusema kwamba Sunnah ni kutonyamaza kitambo kidogo baada ya kumaliza kusoma al-Faatihah kisha baadaye wewe mwenyewe ukanyamaza. Kwa sababu jambo hilo linaingia ndani ya maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لِمَ تَقُولُونَ مَا لَا تَفْعَلُونَ كَبُرَ مَقْتًا عِندَ اللَّـهِ أَن تَقُولُوا مَا لَا تَفْعَلُونَ

“Enyi walioamini!  Kwanini mnasema yale msiyoyafanya? Ni chukizo kubwa kabisa mbele ya Allaah kwamba mnasema yale msiyoyafanya.”[1]

Kama ambavo si sawa kutendea kazi Sunnah ilihali mtu huyohuyo hailinganii katika kwa maneno mazuri na kwa hekima na kwa njia ilionzuri. Kwa hiyo ni lazima kwake kukusanya kati ya mambo mawili.

[1] 61:02-03

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Hudaa wan-Nuur (586)
  • Imechapishwa: 15/12/2020