Kuhusu kukusanya ndugu zake maiti katika nyumba moja  na kuwapokea watu kutoka kila upande, wakawatengenezea chakula, kuwatayarishia viti, kuwasha mataaa na mfano wa hayo, yote hayo yanaenda kinyume na Sunnah na ni kwenda kinyume na yale waliyokuwemo Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Jariyr bin ´Abdillaah al-Bajaliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Tulikuwa tukizingatia kukusanyika kwa familia ya maiti na kutengeneza chakula baada ya mazishi ni aina fulani ya kuomboleza.”[1]

Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walikuwa wakizingatia jambo hilo kuwa ni katika maombolezo. Wao ndio wajuzi zaidi wa ummah juu ya manufaa ya Shari´ah, wabora walioifanyia kazi Shari´ah, wabora wa maono na wenye nyoyo zilizotakasika zaidi. Hakika imethibiti kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Maiti huadbibiwa kwa kule familia yake kuombolezewa.”[2]

Je, kuna yeyote ambaye anaridhia baba yake, mama yake, mvulana wake, msichana wake au mwengine katika jamaa zake kuadhibiwa kwa sababu ya kitendo chake? Je, kuna yeyote ambaye anaridhia kusababisha watu hawa kuadhibiwa? Kama ni mkweli katika kuwapenda basi ahakikishe hasababishi wao kuadhibiwa.

[1] Ahmad (2/204) na Ibn Maajah (1612). ash-Shawkaaniy amesema:

”Cheni yake ya wapokezi ni Swahiyh.” (Nayl-ul-Awtwaar)

[2] al-Bukhaariy (1291) na Muslim (927).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/362-363)
  • Imechapishwa: 20/05/2026