Matanga yana madhara mengi ikiwa ni pamoja na:

1 – Yanawatia uzito watu kwa njia ya kwamba wanalazimika kuhudhuria kutoka kila mahali. Hali inakuwa nzito zaidi ikiwa kuna joto, baridi, mvua na upepo mkali. Pale ilipokuwa kwamba mikusanyiko hii ni mazowea, basi ikawa yule asiyeweza kutokea anatukanywa na kusengenywa na hivyo anakuja kwa kutokupenda kwake. Kuna khatari vilevile akaacha yale mambo muhimu yanayomuhusu na pengine akajiweka khatrarini kwenye barabara.

2 – Mchanganyiko wa wanaume na wanawake. Wanawake wanalia, kuomboleza na kujiombea maangamivu, mambo yanayopingana na subira. Pengine maombolezo yakaenda mbali zaidi katika kufuru. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemlaani mwanamke anayeomboleza na mwanamke anayesikiliza maombolezo na akasema:

“Mwanamke mwenye kuomboleza ikiwa hakutubia kabla ya kufa kwake, basi atafufuliwa siku ya Qiyaamah na huku akiwa amevishwa nguo ya shaba iliyoyeyuka na kanzu ya ukoma.”[1]

3 – Kuharibu pesa katika jambo ambalo halikuwekwa katika Shari´ah. Pengine pesa zinazotumika ni katika mirathi aliyoacha anausia maiti, mirathi ya pesa za mayatima au watoto ambao hawajakomaa kiakili. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu wasia:

فَمَن بَدَّلَهُ بَعْدَ مَا سَمِعَهُ فَإِنَّمَا إِثْمُهُ عَلَى الَّذِينَ يُبَدِّلُونَهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

”Atakayeubadilisha baada ya kuusikia, basi hakika dhambi yake ni juu ya wale watakaoubadilisha. Hakika Allaah ni Mwenye kusikia, Mjuzi wa kila kitu.”[2]

Amesema (Tabaarak wa Ta´ala) amesema kuhusu pesa ya mayatima:

وَلَا تَقْرَبُوا مَالَ الْيَتِيمِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ حَتَّىٰ يَبْلُغَ أَشُدَّهُ

”Wala msiikaribie mali ya yatima – isipokuwa kwa njia ya kuiongeza – mpaka afikie umri wa kukomaa.”[3]

Ni jambo linalotambulika kwamba kutumia mali katika mambo kama haya sio njia moja wapo ya kuiongeza.

4 – Pengine wakaleta msomaji wa Qur-aan ambaye anaisoma kwa njia ya kuwahuzunisha watu. Hakika mambo yalivyo ni kwamba Qur-aan imeteremshwa ili kuzipa nyoyo utulivu na kupoza mahuzuniko. Pengine msomaji Qur-aan akapokea malipo yake kutoka katika mirathi ya maiti. Yule anayesoma Qur-aan kwa ajili ya kupata malipo hapati thawabu kutoka kwa Allaah (Ta´ala), bali anapata madhambi kwa jambo hilo. Kwa msemo mwingine wafiwa wa maiti wanakuwa wamesaidia dhambi hii, wameharibu pesa. Kuna khatari vilevile msomaji huyu anasoma Qur-aan kwa sauti ya juu na watu pembezoni mwake wanazungumza na hawaizingatii Qur-aan. Ni jambo lisilostahiki katika kikao ambacho kunasomwa Qur-aan.

5 – Wakati mwingine watu hukosa swalah ya mkusanyiko, khaswa watu wanapokuwa wengi wakishughulishana na kudhoofika sauti za waadhini. Inatambulika kuwa swalah ya mkusanyiko ni wajibu kwa wanaume.

Kutokana na haya nawashauri ndugu zangu waislamu kuachana na matendo haya na kurejea katika yale waliyokuwemo Salaf. Hakika kheri inapatikana katika mwongozo wao. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Wale waliotangulia mwanzoni ambao ni Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema, Allaah ameridhika nao nao wameridhika Naye na amewaandalia mabustani yapitayo chini yake mito – ni wenye kudumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.”[4]

Punde umekwishajua yale aliyosema Jariyr bin ´Abdillaah al-Bajaliy (Radhiya Allaahu ´anh). Msaada mkubwa wa kuepuka mambo hayo yaliyotajwa mwanafunzi alizingatie suala hili na kuyalinganisha na matendo ya Salaf na awabainishie watu haki ni ipi. Watu wa kawaida ambao wanatafuta haki hawapindi kutokana nayo pale inapowabainikia.

Namwomba Allaah (Ta´ala) atujaalie sote kuwa miongoni mwa wanaolingania katika haki na kuinusuru na miongoni mwa wenye kuona haki kuwa ni haki na wakaifuata na wenye kuona batili kuwa ni batili  na wakajiepusha nayo. Kwani hakika Yeye ni mwingi wa kutoa, Mkarimu. Swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, jamaa zake, Maswahabah zake na wale wote watakaowafata mpaka siku ya Qiyaamah.

Muhammad bin Swaalih al-´Uthaymiyn

1412-01-13

[1] Muslim (934).

[2] 2:181

[3] 17:34

[4] 9:100

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/363-365)
  • Imechapishwa: 20/05/2026