59. Maa´iz bin Maalik ataingia Peponi

Miongoni mwa watu hao ni Maa´iz (Radhiya Allaahu ´anh). Sulaymaan bin Abiy Buraydah amesimulia kutoka kwa baba yake (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Maa´iz bin Maalik alienda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema: “Ee Mtume wa Allaah, nitwahirishe!” Akasema: “Maangamivu ni kwako! Rejea, umwombe Allaah msamaha na utubie Kwake.” Akarejea kitambo si kirefu sana na kusema: “Ee Mtume wa Allaah, nitwahirishe!” Akasema: “Maangamivu ni kwako! Rejea, umwombe Allaah msamaha na utubie Kwake.” Akarejea kitambo si kirefu sana na kusema: “Ee Mtume wa Allaah, nitwahirishe!” Mtume akamjibu tena kama mwanzo. Mara ya nne Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Nikutwahirishe kutokana na nini?” Akasema: “Kutokana na uzinzi.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akauliza: “Je, ni mwendawazimu?” Akapewa khabari kwamba sio mwendawazimu. Akauliza: “Je, amekunywa pombe?” Bwana mmoja akasimama na kuanza kumnusa, lakini hakuhisi kwake harufu ya pombe.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Je, umezini?” Akajibu: “Ndio.” Matokeo yake akaamrisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) apigwe mawe. Baada ya hapo watu wakagawanyika juu yake katika misimamo mawili. Baadhi wakasema: “Ameangamia kwa sababu madhambi yake yamemzunguka.” Wengine wakasema: “Ni tawbah ipi ilio bora kama tawbah ya Maa´iz! Amekuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akauweka mkono wake juu ya mkono wake na kumuomba amuue kwa mawe.” Mada ikawa ni hiyo kwa muda wa siku tatu au nne. Akaja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati walipokuwa wameketi chini, akawasalimia, akaketi chini na kusema: “Muombeeni msamaha Maa´iz bin Maalik.” Wakasema: “Ee Allaah msamehe Maa´iz bin Maalik.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ametubia tawbah ambayo ingeligawanywa kati ya ummah, basi ingeliwaenea wote.”[1]

[1] Muslim (1695).

  • Muhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 138-139
  • Imechapishwa: 21/05/2026