Usifanye chochote ambacho hakikufanywa na Salaf

Kwenda kwa muheshimiwa Shaykh Muhammad bin Swaalih al-´Uthaymiyn

السلام عليكم و رحمة الله و بركاته

Nataraji kuwa utanibainishia hukumu ya Shari´ah katika swali lifuatalo: Mara tu wakati ndugu zangu na ndugu zake mume wangu walipopata khabari za kufariki kwa mtoto wangu wa kiume walikuja kunipa mkono wa pole na kunifariji. Kwa vile nyumba yangu ni ndogo na haiwatoshi wageni wote, nikakodi viti na magodoro nilivyoviweka nje ya nyumbani kwangu. Vilevile nikaweka mataa maeneo hayo yaliyokuwa giza. Baina ya Maghrib na ´Ishaa nikaketi hapo nikipokea wageni hao wanaokuja kutoa ramrirambi. Nyumbani wakapokelewa wageni wanawake. Allaah anajua kuwa sikufanya jambo hilo kwa kukusudia au kwa kuamini kuwa ni jambo limewekwa katika Shari´ah, lakini hiyo ndio hali yangu kama nilivyokutajia. Napenda vilevile kukuashiria kwamba jambo hilo limekuwa ni desturi miongoni mwetu. Hivi sasa imekuwa ni vigumu kuwakatalia wajumbe hao wanaokuja, vinginevyo nakuwa ni mwenye kusemwa vibaya. Aidha nachelea iwapo nitafanya hivo basi kutatokea mpasuko na magomvi kati ya wanafamilia zangu. Je, nilichofanya nimepatia? Je, kitendo hicho kinapingana na radhi za Allaah (Ta´ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Ni kipi cha kufanya katika hali kama hizi?

بسم الله الرحمن الرحيم

و عليكم السلام و رحمة الله و بركاته

Naona kuwa unapaswa kufunga tukio zima haraka iwezekanavyo kwa sababu ni Bid´ah na pia ni kuharibu pesa katika isiyokuwa utiifu. Isitoshe tukio hilo halipelekei katika manufaa ya kidunia. Kutoa rambirambi sio sherehe ya furaha ambayo mataa yanawashwa kwa ajili yake, kuwekwa viti na kupikwa vyakula. Jariyr bin ´Abdillaah al-Bajaliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Tulikuwa tukizingatia kukusanyika kwa familia ya maiti na kutengeneza chakula baada ya mazishi ni aina fulani ya kuomboleza.”[1]

Vilevile imethibiti kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kueleza kwamba maiti huadhibiwa kwa familia yake kumuombolezea.

Ikiwa unakhofia baadhi ya watu kukusema vibaya, basi unatakiwa kuwaeleza kwamba maombolezo ni kwa ajili yako – na mimi sitaki kufanya jambo lolote ambalo halikufanywa na Salaf katika Maswahabah na wale waliowafuata kwa wema (Radhiya Allaahu ´anhum). Ikiwa utasitisha mazowea hayo kwa ajili ya kutafuta radhi za Allaah, basi Allaah atawafanya watu kukuridhia. Hasira zao dhidi yao atazibadilisha kuwa na mapenzi kwako. Vilevile pale watapohudhuria unaweza kuwabainishia kwamba hivi sasa unawakirimu kwa kuwakaribisha, lakini hakuna mikusanyiko mingine baada ya hapo. Allaah akuwafikishe katika kheri na akusaidie juu yake.

Muhammad bin Swaalih al-´Uthaymiyn

1414-10-07

[1] Ahmad (2/204) na Ibn Maajah (1612). ash-Shawkaaniy amesema:

”Cheni yake ya wapokezi ni Swahiyh.” (Nayl-ul-Awtwaar)

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/391-392)
  • Imechapishwa: 24/06/2026