Mgogoro kati ya maimamu wawili al-Bukhaariy na adh-Dhuhliy

al-Hasan bin Muhammad bin Jaabir amesema:

”Nimemsikia Muhammad bin Yahyaa akisema wakati Muhammad bin Ismaa´iyl al-Bukhaariy alipofika Niysaabuur:

”Nendeni kwa bwana huyu mwema na mumsikilize.” Ndipo watu wakaenda kwake na wakaanza kumsikiliza mpaka vikao vya Muhammad bin Yahyaa vikapungua. Akamuonea wivu na ndipo akaanza kumzungumza vibaya.”

Abu Ahmad bin ´Adiyy amesema:

”Nimewasikia jopo la wanachuoni wakinieleza kwamba wakati Muhammad bin Ismaa´iyl al-Bukhaariy alipofika Niysaabuur, watu wakaanza kukusanyika kwake. Baadhi ya wanachuoni wa Hadiyth walipoona hivo, wakamuonea wivu na wakawaambia watu wa Hadiyth: Muhammad bin Ismaa´iyl anasema: ”Matamshi ya Qur-aan yameumbwa.” Hivyo wakampa mtihani katika kikao fulani. Wakati watu walipokusanyika kwake kwenye kikao, akasimama bwana mmoja akasema: ”Ee Abu ´Abdillaah! Unasemaje juu ya matamshi ya Qur-aan? Yameumbwa au hayakuumbwa?”al-Bukhaariy akampuuza na hakumjibu kitu. Bwana yule akamuuliza tena na al-Bukhaariy akafanya alivofanya mara ya kwanza. Aliposema kwa mara ya tatu, al-Bukhaariy akamgeukia na kusema: ”Qur-aan ni maneno ya Allaah na haikuumbwa, matendo ya waja yameumbwa na mitihani ni Bid´ah.” Ndipo bwana yule na wasikilizaji wakafanya ghasia. Mwishowe watu wote wakamtenga na al-Bukhaariy akaketi nyumbani kwake.”

Muhammad bin Muslim Khashnaam amesema:

”Muhammad bin Ismaa´iyl aliulizwa huko Niysaabuur kuhusu matamshi. Akasema: ”´Ubaydullaah bin Sa´iyd amenihadithia: Yahyaa bin Sa´iyd amesema: ”Matendo yote ya waja yameumbwa.” Wakamfanyia fujo na wakamwambia: ”Jirejee kutoka katika maneno hayo ili tuweze kurejea kwako!” Akasema: ”Sintofanya hivo mpaka mje na hoja yenye nguvu zaidi kushinda hoja yangu.” Nimependekezwa na uimara wa Muhammad bin Ismaa´iyl.”

Muhammad bin Yuunus al-Firabriy amesema:

”Nimemsikia Muhammad bin Ismaa´iyl akisema: ”Matendo ya waja yameumbwa. ´Aliy bin ´Abdillaah ametuhadithia: Marwaan bin Mu´aawiyah ametuhadithia: Abu Maalik ametuhadithia, kutoka kwa Rabiy´, kutoka kwa Hudhayfah, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

”Hakika Allaah anamsikia kila mtendaji na kitendo chake.”

Abu Haamid al-A´mash amesema:

“Nilimuona Muhammad bin Ismaa´iyl katika mazishi ya Abu ´Uthmaan bin Marwaan. Pembezoni mwake alikuwa amesimama Muhammad bin Yahyaa [adh-Dhuhliy] akimuuliza kuhusu majina, Kunaa na kasoro za Hadiyth. Muhammad bin Ismaa´iyl akimjibu kama mshale. Baada ya hapo hakukupita mwezi ndipo Muhammad bin Yahyaa akasema: “Yule mwenye kwenda katika vikao vyake basi asije kwetu. Tumejiwa na barua kutoka Baghdaad ya kwamba anasema kuwa matamshi ya Qur-aan yameumbwa na tumemkataza lakini hakataziki. Msimkaribie! Yeyote atakayemkaribia basi asitukaribie!” Muhammad bin Ismaa´iyl akakaa muda fulani ndani ya mji. Halafu baada ya hapo akaenda Bukhaaraa.”

al-Bukhaariy amesema:

”Nimetazama maneno ya mayahudi, manaswara na majusi, lakini sijaona ambaye ni mpotevu zaidi katika ukafiri wake kama Jahmiyyah. Naonelea kuwa yule asiyewakufurisha ni mjinga.”

´Abdur-Rahmaan bin Abiy Haatim amesema katika ”al-Jarh wat-Ta´diyl”:

”Muhammad bin Ismaa´iyl alikuja Rayy mwaka wa 250. Baba yangu na Abu Zur´ah wote wawili wamesikia kutoka kwake. Halafu baada ya hapo Muhammad bin Yahyaa akawaandikia barua ambapo ndani yake alikuwa ameandika kwamba yuko Niysaabuur na anasema kuwa matamshi yake ya Qur-aan yameumbwa.”

Nasema: Ni mamoja waliacha au hawakuacha Hadiyth zake, al-Bukhaariy ni mwaminifu, mwenye kuaminiwa na ni mwenye kutumiwa kama hoja ulimwenguni.

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (12/453-462)
  • Imechapishwa: 28/09/2020