Ufafanuzi kuhusu ni lini imesuniwa kwa msafiri kukusanya na kufupisha

Swali: Nilikuwa msafiri kutokea ar-Riyaadh kwenda katika mji wa mbali na kipindi hicho nilikuwa nafupisha swalah. Siku moja niliazimia kusafiri kwenda katika mji mwingine uliokaribu. Je, inafaa kwangu kukusanya kati ya Maghrib na ´Ishaa kukusanya wakati wa Maghrib au kukusanya wakati wa ´Ishaa? Ikiwa inafaa ni kipi ambacho ni bora?

Jibu: Inafaa kwako kufupisha muda wa kuwa hujarudi katika mji wako kama ambavyo vilevile inafaa kwako kukusanya. Kwa sababu ukusanyaji ni miongoni mwa ruhusa za safari na ufupishaji ni miongoni mwa Sunnah zake zilizokokotezwa sana. Kiasi cha kwamba wako wanachuoni wenye kuona kuwa ufupishaji ni katika mambo ya faradhi ya safari. Wanaona kuwa ni lazima kwa msafiri kufupisha.

Lakini ukiwa katika mji basi ni lazima kwako kuhudhuria swalah za mkusanyiko ukisikia adhaana. Hayo ni kutokana na ueneaji wa dalili zinazomuwajibishia yule mwenye kusikia adhaana ahudhurie. Ukihudhuria na ukaswali pamoja na imamu ambaye ni mkazi basi ni lazima kwako kuswali kikamilifu.

Ama kuhusu ukusanyaji inafaa kwako kukusanya midhali bado ni msafiri. Lakini bora kuhusu ukusanyaji ni mtu asikusanye isipokuwa akihitajia kufanya hivo. Kwa mfano safari imeviwa kwelikweli na hivyo akapendelea kuendelea na safari yake, katika hali hii anaweza kukusanya katika ule wakati wa mwanzo au akachelewesha katika ule wakati wa pili kutegemea na vile itavyokuwa sahali kwake.

Kujengea juu ya haya ukitaka kusafiri kutoka ar-Riyaadh na kwenda katika mji mwengine uliokaribu na ar-Riyaadh na hutaki kukatisha safari yako, basi hakuna neno ukakusanya mkusanyo wa kutanguliza hapohapo mjini kabla ya kufika katika mji unapoelekea. Vilevile inafaa kwako kuchelewesha na ukakusanya mkusanyo wa kuchelewesha mpaka ufike katika mji wa pili ikiwa utafika kabla ya kuisha wakati wa ile swalah ya pili. Vinginevyo utakusanya wakati wa safari yako.

Muhimu ni kwamba inafaa kwa msafiri kukusanya japo kuacha kufanya hivo ndio bora zaidi muda wa kuwa hahitajii kufanya hivo. Hapo ndipo itakuwa imesuniwa na imependekezwa. Bora ni kukusanya mkusanyo wa kutanguliza au mkusanyo wa kuchelewesha kwa kutegemea na vile itavyokuwa rahisi kwako. Bora juu yako ni kutegemea na vile itavyokuwa rahisi safarini mwako.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (18) http://binothaimeen.net/content/6824
  • Imechapishwa: 12/09/2021