Makatazo ya kuchora viumbe vilivyo na roho

Swali: Je, kuchora viumbe wenye roho kama wanyama na mtu kwenye karatasi na kuzipaka rangi ni kitu kinachojuzu? Je, ni jambo linaingia ndani ya ujumla wa Hadiyth al-Qudsiy ambapo Allaah (Ta´ala) amesema:

ومن أظلم ممن ذهب يخلق كخلقي، فليخلقوا ذرة أو ليخلقوا حبة أو ليخلقوا شعيرة

“Ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule ambaye anajaribu kuumba mfano wa viumbe Wangu? Hebu waumbe mdudu chungu, waumbe punje ya nafaka au waumbe chembe ya shayiri.”?

Jibu: Ndio, ni jambo linaingia ndani ya Hadiyth hii. Lakini uumbaji umegawanyika aina mbili:

1 – Uchoraji wa mwili wa kisifa. Hizi ni zile picha zinazochorwa za kimwili.

2 – Uchoraji wa sifa na si mwili. Hizi ni zile picha zinazochorwa.

Aina zote mbili hizi zinaingia ndani ya Hadiyth hii. Kuchora sifa ni kama kuchora kiwiliwili ingawa kuchora kiwiliwili ndio khatari zaidi kwa sababu ni jambo limekusanya kati ya mambo mawili; kuchora mwili na wasifu wake. Dalili ya hilo ni ule ueneaji na kwamba ni kuchora kwa mkono. Ni mamoja ni kiwiliwili au kimechorwa kwa rangi. Ni jambo lenye kuenea. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewalaani wenye kutengeneza picha. Ueneaji wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwalaani watengeneza picha ni dalili inafahamisha kwamba hakuna tofauti kati ya picha za kiwiliwili na zilizotiwa rangi ambazo zinachorwa kwa kutiwa rangi.

Lililo salama zaidi na bora kwa muumini ni yeye kujiepusha na utata. Lakini huenda mtu akauliza kwamba bora si ni kufuata yale yaliyofahamishwa na andiko na kufuata kile ambacho kikubwa zaidi? Ni sahihi kwamba kufuata kilicho salama zaidi ni kufuata yale yaliyofahamishwa na andiko na si kufuata kile ambacho ni kikubwa zaidi. Lakini kunapopatikana andiko lenye kuenea ambalo linaweza kufasiriwa kwa njia nyingi basi lililo salama zaidi ni kutendea kazi lile lililoenea zaidi, jambo ambalo  linahusu Hadiyth zinazozungumzia picha. Kwa hivyo haijuzu kwa mtu kuchora picha za kiumbe kilicho na roho. Haijalishi kitu ni mtu au mnyama mwengine. Kwa sababu ni jambo linaloingia ndani ya kulaaniwa watengeneza picha.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (18)
  • Imechapishwa: 12/09/2021