Uchokozi dhidi ya Uislamu na waislamu – lakini Uislamu utaendelea kubaki

Moja katika alama za utume ni wingi wa fitina katika zama za mwisho, kama alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Elimu itanyanyuliwa, ujinga utaenea na fitina zitakuwa nyingi.”[1]

Walinganizi kwa Allaah kuitwa kuwa ni vibaraka ni moja katika alama hizo. Abu Hurayrah na Anas wamesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu watafikiwa na zama za hadaa ambazo mwongo atasadikishwa na mkweli atakadhibishwa, khaini ataaminiwa, mwaminifu atazingatiwa kuwa khaini na Ruwaybidhwah atazungumza.” Wakasema: “Ni nani Ruwaybidhwah? Ndipo akasema: “Ni mpumbavu anayezungumza mambo ya ummah.”[2]

Umesema kweli, ee Mtume wa Allaah. Maadui wa Allaah wamezidi kuwa wakali, vyombo vyao vya khabari kushambulia Uislamu na waislamu na wakati mwingine kuwatuhumu vibaraka na ukhaini, wakati mwingine kuwatuhumu upumbavu, wakati mwingine kuwatuhumu kuwa na msimamo mkali, itikali kali na watu wanaoshikamana na misingi. Hakuna chochote kinachowafanya watu kuikimbia dini takasifu isipokuwa wamekitumia. Kama isingelikuwa Allaah kuihifadhi dini hii, basi isingelikuwepo, lakini Allaah anasema:

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ

“Hakika Sisi Tumeteremsha Ukumbusho huu na hakika Sisi bila shaka ndio Tutakaouhifadhi!”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hatokuacha kuwepo kikundi kutoka katika ummah wangu hali ya kuwa ni chenye kushinda juu ya haki. Hakitodhurika na wale wenye kuwakosesha nusura wala wale wenye kwenda kinyume nao mpaka ifike amri ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) wakiwa katika hali hiyo.”[4]

Kwa ajili hiyo wanazuoni wanapaswa kutegemea ahadi ya Allaah na kuwabainishia watu dini ya Allaah, kwa sababu kuficha elimu ni jambo la khatari:

إِنَّمَا يَأْمُرُكُم بِالسُّوءِ وَالْفَحْشَاءِ وَأَن تَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ

“Hakika si vyengine isipokuwa anakuamrisheni maovu na machafu na mseme juu ya Allaah yale msiyoyajua.”[5]

[1] al-Bukhaariy na Muslim.

[2] Ibn Maajah (4036) na Ahmad (2/291).

[3] 15:9

[4] Muslim (1920).

[5] 2:169

  • Muhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Mu´aanid, uk. 5-6
  • Imechapishwa: 21/01/2025