Tofauti ya kusoma na kujidanganya

Swali: Unamnasihi nini mwanafunzi mpya anayeanza? Ni vitabu vyepi unavyompendekeza?

Jibu: Kusoma hakuhusiani na kusoma na kuhifadhi vitabu hata kama vitakuwa vingi. Kusoma inahusiana na kudurusu na kuchukua elimu kutoka kwa wanachuoni kupitia katika masomo ya nidhamu kwa njia ya shule, masomo na vyuo au kwenye misikiti na mizunguko ya kielimu; huku ndio kusoma. Ama kusoma na kuhifadhi vitabu na Hadiyth ni jambo ambalo linaweza kumdhuru mwenye nalo. Anafikiria kuwa ni msomi wakati uhakika wa mambo hafahamu hata kile anachokisoma. Hanufaiki kwa lolote. Kusoma hakuhusiani na kusoma vitabu peke yake; kusoma kunapitika chini ya wanachuoni popote watapokuwa. Wanatakiwa kuendewa, mtu anatakiwa kusafiri kuwaendea. Ambaye anataka kutafuta elimu hana njia nyingine isiyokuwa hii:

“Yule mwenye kuchukua njia akitafuta elimu basi Allaah atamsahilishia kwayo njia ya kwenda Peponi.”[1]

Amechukua njia. Hakukaa na kusoma na kuhifadhi. Anasafiri kwenda kwa wanachuoni, anawatafuta, anachukua elimu kutoka kwao. Mkisoma historia ya wanachuoni waliotangulia, kama mfano wa Imaam Ahmad na al-Bukhaariy, mtaona jinsi walivyosafiri katika miji ya mbali ili kukutana na wanachuoni na kusoma kwao. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَمَا كَانَ الْمُؤْمِنُونَ لِيَنفِرُوا كَافَّةً ۚ فَلَوْلَا نَفَرَ مِن كُلِّ فِرْقَةٍ مِّنْهُمْ طَائِفَةٌ لِّيَتَفَقَّهُوا فِي الدِّينِ وَلِيُنذِرُوا قَوْمَهُمْ إِذَا رَجَعُوا إِلَيْهِمْ لَعَلَّهُمْ يَحْذَرُونَ

“Na haiwapasi waumini watoke wote pamoja kwenda [kupigana vita vya jihaad]. Basi kwanini lisitoke katika kila kundi miongoni mwao, kundi [moja] wajifunze dini na ili waonye watu wao watakaporejea kwao ili wapate kutahadhari.” (09:122)

Bi maana kutafuta elimu. Ni lazima kwa mtu atoke asafiri kwa ajili ya kutafuta elimu popote ilipo. Ama kujaza nyumba vitabu, kusoma na kuhifadhi sio kusoma. Huku ni kujidanganya. Wanaojifanya wanachuoni na wajinga wamejidanganya wenyewe, kufanya mambo ya kijinga na kutoa fatwa pasi na elimu!

[1] Muslim (7052).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Tafsiyr-ish-Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (22) http://www.alfawzan.af.org.sa/sites/default/files/tafsirayat-05-07-1435-01.mp3