Tofauti kati ya Ahl-us-Sunnah na Ahl-ul-Bid´ah katika kuwapa watu vyeti vya Pepo na Moto

Imaam at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hatumkatii yeyote katika wao Pepo wala Moto.”

Katika hili Ahl-us-Sunnah wanatofautiana na Ahl-ul-Bid´ah. Khawaarij wanamshuhudilia Moto kila mtenda dhambi. Kadhalika Mu´tazilah ambao wanamshuhudilia Moto mwenye kufa katika dhambi kubwa na kwamba ametoka katika imani na wakati huo huo hakuingia katika kufuru. Hili ndio lengo la kuingiza mambo haya katika vitabu vya ´Aqiydah.

Kwa kifupi ni kwamba, mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah katika mlango huu ni wenye kukomeka inapokuja mtu kwa dhati yake, kwa maana ya kwamba hawamshuhudilii yeyote Pepo wala Moto isipokuwa kwa ujuzi – nao ni wale walioshuhudiliwa na Maandiko – kwa sababu uhakika umejificha. Mwenye kufa hatuwezi kutambua uhakika wake. Lakini hata hivyo tunataraji mema kwa watu wema na tunachelea kwa watenda maovu. Kanuni katika hili ni: kila ambaye tunaona anafanya matendo mema na amenyooka katika kumtii Allaah, basi tunatarajia kwake mema pasina kumshuhudilia Pepo. Upande mwingine tunayemwona anafanya maovu na madhambi makubwa, tunachelea kwake Moto na wala hatushuhudilii kuwa ni mwenye kuingia Motoni. Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (01/540)
  • Imechapishwa: 19/05/2020