Thawabu kwa wale wenye kusubiri

Swali: Tunaomba utueleze yale ambayo Allaah amewaandalia wale wenye kusubiri duniani na Aakhirah na wale wenye kumtii Allaah?

Jibu: Allaah amewaumba viumbe ili wamwabudu Yeye pekee hali ya kuwa hana mshirika na akawaamrisha jambo hilo pale aliposema (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.”[1]

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu ambaye amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kumcha.”[2]

´Ibaadah hii ambayo wameumbiwa na kuamrishwa kwayo ni kutii maamrisho Yake na kukomeka na makatazo Yake na kukithirisha kumtaja. Msingi wa ´ibaadah hii ni kumpwekesha (Subhaanah) kwa kumwomba, kumwogopa, kumtaraji na kumtakasia nia katika ´ibaadah zote kukiwemo swalah, funga na mengineyo.

Allaah amewaahidi kheri nyingi na mwisho wenye kusifiwa duniani na Aakhirah. Allaah amewaahidi huko Aakhirah kuwatunuku Pepo na heshima. Amesema (Ta´ala):

فَاصْبِرْ ۖ إِنَّ الْعَاقِبَةَ لِلْمُتَّقِينَ

“Basi subiri, hakika mwisho mwema ni kwa wenye kumcha Allaah.”[3]

وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

“Wabashirie wenye kusubiri – wale ambao unapowafika msiba husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.” – [wafikishie ya kwamba] hao zitakuwa juu yao barakah kutoka kwa Mola wao na rahmah; na hao ndio wenye kuongoka.”[4]

إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ

“Hakika si venginevyo wale wenye kusubiri watalipwa kikamilifu ujira wao pasi na hesabu.”[5]

مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً ۖ وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Yule mwenye kutenda mema katika wanamme au wanawake – ilihali ni muumini – basi Tutamhuisha maisha mazuri na tutawalipa ujira wao kwa mazuri zaidi ya yale waliyokuwa wakitenda.”[6]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mtu hajapewa zawadi nzuri na yenye wasaa zaidi kuliko subira.”

“Ajabu iliyoje juu ya jambo la muumini. Hakika mambo yake yote huwa ni kheri. Asifikwa na kitu cha kufurahisha basi hushukuru na ikawa ni kheri kwake. Na akifikwa na kitu cha kusononesha basi husubiri na ikawa ni kheri kwake – na hilo haliwi kwa yeyote isipokuwa kwa muumini tu.”

Mvuta subira ana mwisho wenye kusifiwa duniani na Aakhirah. Au pia ana Pepo na heshima huko Aakhirah akisubiri juu ya kumcha na kumtii Allaah (Subhaanah) na akasubiri juu ya yale aliyopewa mtihani kwayo ambayo ni ukata wa maisha, umasikini, ufukara, magonjwa na mengineyo. Allaah (Subhaanah) amesema:

لَّيْسَ الْبِرَّ أَن تُوَلُّوا وُجُوهَكُمْ قِبَلَ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ وَلَـٰكِنَّ الْبِرَّ مَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالْكِتَابِ وَالنَّبِيِّينَ وَآتَى الْمَالَ عَلَىٰ حُبِّهِ ذَوِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ وَالسَّائِلِينَ وَفِي الرِّقَابِ وَأَقَامَ الصَّلَاةَ وَآتَى الزَّكَاةَ وَالْمُوفُونَ بِعَهْدِهِمْ إِذَا عَاهَدُوا ۖ وَالصَّابِرِينَ فِي الْبَأْسَاءِ وَالضَّرَّاءِ وَحِينَ الْبَأْسِ ۗ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ صَدَقُوا ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُتَّقُونَ

“Si wema pekee kwa nyinyi kuelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi, lakini wema khaswa ni yule mwenye kumuamini Allaah na siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii na akawapa mali pamoja na kuipenda kwake jamaa wa karibu na mayatima na masikini na msafiri na waombao na katika kukomboa watumwa na akasimamisha swalah na akatoa zakaah na watekelezea ahadi zao wanapoahidi na wanaosubiri katika shida na dhara na wakati wa njaa na katika vita – basi hao ndio waliosadikisha na hao ndio wenye kumcha Allaah.”[7]

Subira na kumcha Allaah mwisho wake ni mzuri katika hali zote. Amesema (Ta´ala) juu ya waumini pamoja na maadui wao:

وَإِن تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا لَا يَضُرُّكُمْ كَيْدُهُمْ شَيْئًا ۗ إِنَّ اللَّـهَ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطٌ

“Mkisubiri na mkaogopa haitokudhuruni chochote katika hila zao. Hakika Allaah ni mwenye kuyazunguka yote wayatendayo.”[8]

[1] 51:56

[2] 02:21

[3] 11:49

[4] 02:155-156

[5] 39:10

[6] 16:97

[7] 02:177

[8] 03:120

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/2017/اجر-الصابرين-في-الدنيا-والاخرة
  • Imechapishwa: 23/05/2021