Sharti ya tatu [ya tawbah] ni mtu kujivua na dhambi aliyomo. Hii ni sharti muhimu zaidi. Kujivua na dhambi, ikiwa dhambi ni mtu kuacha jambo la wajibu, basi kujivua na dhambi hiyo ni kwa yeye kutenda jambo hilo. Kwa mfano mtu si mwenye kutoa zakaah na sasa anataka kutubia kwa Allaah ni lazima atoe zakaah ya miaka iliyopita ilihali alikuwa hatoi. Ikiwa mtu alikuwani wenye kupuuzia kutekeleza haki za wazazi, ni wajibu kwake kusimama kwa kuwatendea wema. Ikiwa ni mwenye kufanya mapungufu kwa kuunga kizazi, ni wajibu kwake kuwaunga jamaa tzake.

Ama ikiwa maasi ni kwa kufanya mambo ya haramu, lililo la wajibu ni yeye kujivua na dhambi hiyo haraka iwezekanavyo na asibaki katika dhambi hiyo kwa muda hata mdogo. Kwa mfano mtu ni miongoni mwa wanaokula ribaa, basi ni wajibu kujikwamua na kula ribaa kwa kuiacha, kujitenga nayo mbali, kutoa vile alivyovichuma kwa njia ya ribaa. Ikiwa maasi ya mtu ni kufanya ghushi, kuwadanganya watu na kufanya khiyana, basi lililo la wajibu juu yake ni kujivua na jambo hilo. Ikiwa alichuma mali kwa njia hii ya haramu, basi lililo la wajibu ni kurudisha mali hiyo kwa mmiliki. Ikiwa ni usengenyi, basi lililo wajibu ni yeye kujivua na kuwasengenya watu na kuwavunjia heshima zao. Ama mtu kusema kuwa ametubia kwa Allaah ilihali bado ni mwenye kuendelea kuacha ya wajibu au kufanya jambo la haramu, tawbah hii haikubaliwi. Bali tawbah hii ni kama kufanyamaskhara na Allaah (´Azza wa Jall). Vipi utatubu kwa Allaah (´Azza wa Jall) ilihali wewe bado ni mwenye kuendelea kumuasi? Lau utakuwa ni mwenye kutaamiliana na watu na unasema kuwa umetubu, umejuta na hutorudi, lakini wakati huohuo ndani ya moyo wako umenuia kuwa utarudi na baadaye ukarudi. Katika hali hii utakuwa ni mwenye kufanya mashkhara na mtu huyu. Tusemeje juu ya Allaah, Mola wa walimwengu? Mtu mwenye kutubu kikweli ni yule mwenye kujivua na dhambi.

Jambo lenye kushangaza ni kwamba utaona kuna watu ambao wanauguwa kwa ribaa, lakini yeye mwenyewe anakula ribaa. Mwingine anauguwa kwa kusengenya na kula nyama za watu, lakini yeye ni miongoni mwa watu wanaosengenya sana. Mwingineanauguwa kwa kusema uongo na kupoteza amana za watu, lakini hakuna msema uongo na mpoteza amana mkubwa kama yeye.

Kwa hali yoyote ni lazima kwa mtu kujivua na dhambi ambayo ametubia kwayo. Ikiwa hakujivua na dhambi hiyo, basi tawbah yake ni yenye kurudishwa na haitomfaa lolote mbele ya Allaah (´Azza wa Jall).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/86-88)
  • Imechapishwa: 30/01/2023