Tamko la Isti´aadhah kamili zaidi kabla ya kuanza kusoma Qur-aan

Swali: Kuna Shaykh mmoja amesema kuanza kisomo kwa kusema:

أَعوذ بالله السميع العليم من الشَّيْطانِ الرَّجِيمِ من هَمْزِهِ ونَفْخِهِ ونَفثِه

“Ninajilinda kwa Allaah, Mwenye kusikia, Mjuzi, kutokamana na shaytwaan aliyefukuzwa; upilizaji wake, jeuri yake na ushairi wake.”

ni kitu maalum ndani ya swalah. Je, haya ni kweli?

Jibu: Hadiyth zilizopokelewa zote ni kuhusu ndani ya swalah. Lakini hapana neno kuzibeba nje ya swalah. Ni kama mfano wa kusema ”Aamiyn”. Jambo ndani yake linahusu ubora. Ambaye atafungua kisomo chake kwa kusema:

أَعُوذُ باللهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيم

“Ninajilinda kwa Allaah na shaytwaan aliyefukuzwa.”

amefanya jambo la faradhi. Na ambaye atafungua kisomo chake kwa kusema:

أَعوذ بالله السميع العليم من الشَّيْطانِ الرَّجِيمِ من هَمْزِهِ ونَفْخِهِ ونَفثِه

“Ninajilinda kwa Allaah, Mwenye kusikia, Mjuzi, kutokamana na shaytwaan aliyefukuzwa; upilizaji wake, jeuri yake na ushairi wake.”

amefanya sunnah. Jambo linazunguka kati ya lazima na sunnah. Ama kusema kuwa kitu hicho ni maalum ndani ya swalah hakuna dalili juu ya umaalum kwa nisba ya wanazuoni hapo kale. Ninachokusudia ni kusema, ukirejea kitabu cha Ibn-ul-Jawziy na wengineo – siwakumbuki – utaona kuwa anataja Isti´aadhah kwa tamko hilo kamili. Hafungamanishi na kusema kuwa ni ndani ya swalah peke yake. Ni miongoni mwa adabu za kusoma Qur-aan. Kuomba ulinzi kwa tamko hilo ndio kamili zaidi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sa-altu Abiy, uk. 45-46
  • Imechapishwa: 03/07/2022