Kuleta Takbiyr katika masiku ya Tashriyq baada ya vipindi vitano vya swalah ni jambo limehifadhiwa kutoka kwa Maswahabah akiwemo ´Umar na Maswahabah wengine (Radhiya Allaahu ´anhum). Imepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), hata hivyo katika cheni yake ya wapokezi kuna unyonge. Kadhalika kuleta Takbiyr katika yale masiku kumi ya Dhul-Hijjah kuanzia siku yake ya kwanza. Yote haya yamesuniwa. Imepokelewa kutoka kwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). ´Umar na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) walikuwa wakitoka kwenda sokoni katika masiku kumi ambapo wanaleta Takbiyr na watu nao wanaleta Takbiyr kwa sababu ya Takbiyr yao.

Maswahabah akiwemo ´Umar walikuwa wakileta Takbiyr baada ya vipindi vitano vya swalah kuanzia ile siku ya kwanza ya ´Arafah mpaka ile siku ya mwisho ya Tashriyq. ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) alikuwa akileta Takbiyr ndani ya hema lake Minaa ili watu wasikie nao walete Takbiyr baada ya Takbriy yake. Kwa hivyo kuleta Takbiyr ni jambo limesuniwa na sio wajibu. Ni Sunnah siku ya ´Arafah, siku ya kuchinja na yale masiku ya kuchinja kwa njia isiyofungamana na kwa njia ya kufungamana kama vile baada ya vipindi vya swalah na sehemu nyingine ya wakati wa mchana na usiku. Ama siku ya nane na masiku mengine ya Dhul-Hijjah kabla yake, ni Takbiyr isiyofungamana na haikufungamanishwa na swalah. Bali ni Takbiyr kwa njia ya isiyofungamanishwa kuanzia siku ya kwanza ya Dhul-Hijjah mpaka ule usiku wa tarehe tisa ya Dhul-Hijjah. Takbiyr hii ni yenye kuachiwa. Mtu ataleta Takbiyr akiwa njiani, nyumbani kwake na kitandani mwake. Vivyo hivyo yale masiku ya mwisho ya ´Arafah na baada yake waislamu wanatakiwa kuleta Takbiyr wakiwa njiani, misikitini, masokoni, baada ya vipindi vitano vya swalah katika zile siku tano za mwisho za siku ya ´Arafah na baada yake. Kikosi kikubwa cha wanazuoni wanaona kuwa ni Sunnah tu.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/8774/حكم-التكبير-ايام-عيد-الاضحى-وصيغته
  • Imechapishwa: 11/06/2024