Swalah ya mgonjwa kwa macho na kidole

Mtu akiwa mgonjwa basi tunamwambia yale ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia ´Imraan bin Huswayn (Radhiya Allaahu ´anh):

”Swali kwa kusimama. Usipoweza, kwa kukaa. Usipoweza, lalia bavu.”[1]

Alimwamrisha kuswali kwa kuashiria kwa kichwa.

Kuhusu kuswali kwa kuashiria kwa kidole, sijui mwanachuoni yoyote mwenye maoni hayo. Wala sitambui kuwa jambo hilo lina msingi katika Sunnah. Ni kitu kisichokuwa na maana. Ni utikisikaji uliochukizwa. Kitendo hicho sio Sunnah na wala hakikuwekwa katika Shari´ah.

Kuhusu kuashiria kwa macho, wapo baadhi ya wanazuoni wenye maoni hayo. Wamesema asipoweza kuashiria kwa kichwa chake basi aashirie kwa macho. Katika hali hii afumbe macho zaidi katika Sujuud kuliko anavofanya katika Rukuu´.

Kuashiria kwa kidole ni kitu kimetangaa kwa watu wasiokuwa na elimu. Yule mwenye kufanya hivo ni mjinga na hakuna kinachomlazimu. Haimlazimu kuirudia swalah yake.

Pindi wanafunzi wanapowaona watu wa kawaida wanafanya kitu ambacho hakikuwekwa katika Shari´ah, basi wanatakiwa kufanya bidii kuwazindua juu ya jambo hilo. Watu wa kawaida wanachotaka ni haki, lakini ni wajinga. Wakinyamaziwa mambo haya basi wanaendelea juu yake. Lakini wakizinduliwa katika vikao, khutbah, mawaidha na mihadhara, basi Allaah hunufaisha kupitia mtu huyu.

[1] al-Bukhaariy (1117).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (4 B)
  • Imechapishwa: 07/10/2021