Sunnah ni kusoma Suurah ndefu zaidi katika Rak´ah ya kwanza kuliko ya pili

Swali: Ni ipi hukumu endapo imamu atasoma kwa mfano katika Rak´ah ya kwanza “al-Ikhlaasw” kisha katika ya pili akasoma “adh-Dhwuhaa”?

Jibu: Hakuna neno kwa imamu akisoma katika Rak´ah ya kwanza fupi kuliko ile anayosoma katika ya pili. Kutokana na ueneaji wa maneno ya Allaah (Subhaanah):

فَاقْرَءُوا مَا تَيَسَّرَ مِنْهُ

“Basi someni kile kilicho chepesi humo.”[1]

Pia kutokana na ueneaji wa maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia yule aliyeswali kimakosa:

“Unaposimama katika swalah basi eneza wudhuu´, kisha elekea Qiblah na useme “Allaahu Akbar” na kisha usome kile kitachokuwa chepesi kwako kutoka katika Qur-aan.”

Katika tamko jingine imekuja:

“… kisha usome mama wa Qur-aan na kile unachotaka.”

Lakini kwa kufanya hivo ameacha lile ambalo ni bora zaidi. Kwa sababu Sunnah iliyothibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutoka katika maneno na matendo yake inafahamisha kuwa Sunnah kwa imamu na ambaye anaswal peke yake asome katika Rak´ah ya kwanza ndefu zaidi kuliko katika Rak´ah ya pili. Hayo atayafanya katika swalah zote tano. Kuhusu maamuma ni mwenye kumfuata imamu wake.

[1] 73:20

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (11/82-83)
  • Imechapishwa: 11/10/2021