Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Hakuna aibu kwa yule mwenye kudhihirisha madhehebu ya Salaf, akajinasibisha nayo na akajitukuza kwayo. Bali ni wajibu kumkubalia hilo kwa makubaliano kwa sababu madhehebu ya Salaf si jengine isipokuwa ni haki.”[1]

Zingatia maneno ya Shaykh-ul-Islaam ambayo aliyazungumza miaka 800 ya nyuma. Kana kwamba anamraddi bwana mmoja anayeishi hii leo na anayejinasibisha na elimu. Mtu huyo amesema:

“Yule mwenye kumuwajibishia mtu mwingine kuwa Ikhwaaniy, Salafiy, Tabliyghiy au Suruuriy anatakiwa kuambiwa atubie. Akitubia ni sawa na vinginevyo auliwe.”

Ameyasema katika kanda ulioenezwa kwa vijana ulio na kichwa cha khabari “Firr min al-Hiziyyah Firaarak min al-Asad”.

Ametakasika Allaah kutokana na mapungufu! Ni vipi anaweza kujijuzishia yeye mwenyewe kutaja mfumo wa Salaf wa haki pamoja na mifumo na mapote haya yaliyozushwa na ya kipotofu? Swali langu kwa mtu huyu anayeishi katika nchi ya Tawhiyd na amechukua cheti cha pili katika Hadiyth na hivi karibuni amepata cheti cha udaktari: Awe kitu gani kama si Salafiy? ´Allaamah Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) aliulizwa:

“Unasemaje kuhusiana na mwenye kujiita “Salafiy” au “Athariy”? Je, ni kujitakasa?

Akajibu (Rahimahu Allaah):

“Haina neno ikiwa kama kweli ni Athariy au Salafiy. Kama ambavo baadhi ya Salaf walikuwa wakisema fulani ni “Salafiy” na “Athariy”. Kujitakasa kwa lazima. Kujitakasa kwa lazima.”[2]

Shaykh Bakr Abu Zayd amesema:

“Inaposemwa Salaf, Salafiyuun au mfumo wao ambao ni Salafiyyah, inahusiana na kujinasibisha kwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) na wale wote waliowafuata kwa wema pasi na yule aliyepinda katika matamanio yake… Wale walioshikamana imara na mfumo wa kinabii ananasibishwa na watangu wake wema katika hilo. Ndio maana wanaitwa “Salaf” na “Salafiyyuun”. Yule mwenye kujinasibisha na wao anaitwa “Salafiy”. Kutokana na hilo neno Salaf ni wale wema waliotangulia. Msemo huu unajumuisha kila yule mwenye kuwaiga Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) ikiwa  ni pamoja na watu wa zama zetu, hivyo ndivyo wanavosema wanazuoni. Sio unasibishaji wa mielekeo inayoenda kinyume na Qur-aan na Sunnah. Sio unasibishaji ambao kwa wakati hata mmoja umeenda kinyume na karne za kwanza; bali umetoka kwao na pamoja nao. Licha ya hivyo mtu hawezi kusema hivo kwa wale walioenda kinyume nao kwa jina au mwelekeo hata kama wataishi kati yao na wao.”[3]

Amesema vilevile:

“Kuwa Salafiy katika njia iliyonyooka.”[4]

Unasibishaji huu umetajwa katika vitabu vya historia na vya wasifu. Imaam adh-Dhahabiy amesema kuhusu Muhammad bin Muhammad al-Bahraaniy:

“Alikuwa ni mtu wa dini, mwema na Salafiy.”[5]

Amesema kuhusu Ahmad bin Ahmad bin Ni´mah al-Maqdisiy:

“Alikuwa ni mwenye kushikamana na ´Aqiydah ya Salaf.”[6]

Kujinasibisha na Salaf ni jambo la lazima ili mtu Salafiy aweze kujitofautisha na yule mwenye kujificha na ili kila yule asiyetaka kujinasibisha na wao na kufuata mfumo wao aweze kutumbukia kwenye utatizi. Pindi mielekeo iliyopinda inakuwa mingi na vyama vya mapote potevu na vyenye kupotosha vinajitokeza, basi Ahl-ul-Haqq wanajinasibisha waziwazi na Salaf ili kujitenga mbali na wale wenye kwenda kinyume. Allaah (Ta´ala) amesema kumwambia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na waumini:

فَإِن تَوَلَّوْا فَقُولُوا اشْهَدُوا بِأَنَّا مُسْلِمُونَ

“Wakikengeuka, basi semeni: “Shuhudieni kwamba sisi ni waislamu.””[7]

وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلًا مِّمَّن دَعَا إِلَى اللَّـهِ وَعَمِلَ صَالِحًا وَقَالَ إِنَّنِي مِنَ الْمُسْلِمِينَ

“Na nani mwenye neno nzuri zaidi kuliko yule anayelingania katika kumwamini Allaah, akatenda mema na akasema: “Hakika mimi ni miongoni mwa waislamu.”[8]

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي ۖ وَسُبْحَانَ اللَّـهِ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ

“Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah, juu ya ujuzi na umaizi – mimi na anayenifuata. Utakasifu ni wa Allaah na mimi si miongoni mwa washirikina.”[9]

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (04/149)

[2] Kutoka katika kanda “Haqq-ul-Muslim” 1413/01/16 Twaaif

[3] Hilyatu Twaalib-il-´Ilm, uk. 08

[4] Hilyatu Twaalib-il-´Ilm, uk. 08

[5] Mu´jam-ush-Shuyuukh (02/280)

[6] Mu´jam-ush-Shuyuukh (01/34)

[7] 03:64

[8] 41:33

[9] 12:108

  • Mhusika: Shaykh Jamaal bin Furayhaan al-Haarithiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 37-40
  • Imechapishwa: 14/05/2024