Sharti za kufaa kupandikiza na kutunga mimba

Barua

بسم الله الرحمن الرحيم

السلام عليكم و رحمة الله و بركاته

Nilichofahamu kupitia barua yenu ni kwamba yai la mwanamke linawekwa kwenye mrija kisha linatungishwa kwa manii ya mwanamme. Baada ya hapo yai la mwanamke linarudishwa kwenye kifuko cha uzazi wa mwanamke ili upandikizaji uchukue mkondo wake.

1 – Kitendo hicho hakijuzu ikiwa hakuna haja. Kwa sababu upasuaji kama huo unapelekea kufunua uchi pasi na haja. Aidha kuna khatari, hata kama ni katika siku zijazo za mbali, ya mirija kubadilishwa au kuambukizwa. Ukiongezea ya kwamba kuyaacha mambo juu ya maumbile yake kama alivyoumba Allaah ni ukamilifu zaidi katika kufanya adabu na Allaah. Hivyo ndio bora na manufaa zaidi kuliko njia zinazozuliwa na viumbe ambazo pengine mwanzo wake ukaonekana mzuri lakini baada ya ikaja kubainika kufeli kwake.

2 – Ikiwa kuna haja ya kitendo hicho basi naona kuwa kitafaa kwa kutimia sharti tatu:

1 – Upandikizaji wa mimba uwe kwa manii ya mume na si mwengine yeyote. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَاللَّـهُ جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَجَعَلَ لَكُم مِّنْ أَزْوَاجِكُم بَنِينَ وَحَفَدَةً

”Allaah amekufanyieni wake wanaotokamana na nyinyi wenyewe na amekufanyieni katika wake zenu watoto na wajukuu.”[1]

Watoto wanatakiwa kutoka kwa mume peke yake.

2 – Manii ya mume yatolewe kwa njia inayoruhusiwa kupitia kustarehe na mke wake, ima kupitia kucheza kwenye mapaja au kwa mkono wake.

3 – Ni lazima mirija iwekwe kwenye kifuko cha uzazi wa mke wake na haijuzu kuiweka kwa mwanamke mwingine kwa hali yoyote. Kwa sababu haijuzu kuyaweka manii ya mwanamme kwenye kifuko cha uzazi wa mwanamke ambaye si halali kwake. Allaah (Ta´ala) amesema:

نِسَاؤُكُمْ حَرْثٌ لَّكُمْ فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أَنَّىٰ شِئْتُمْ

“Wake zenu ni konde kwenu. Hivyo ziendeeni konde zenu vyovyote mpendavyo.”[2]

Konde la mwanamme ni yule mke wake na si mwingine. Qur-aan, Sunnah na maafikiano vimefahamisha kuwa mjakazi ana hukumu moja kama mke katika hali hiyo.

[1] 16:72

[2] 2:223

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/27-28)
  • Imechapishwa: 06/09/2022