Rasta wenye kuachia nywele si wakweli katika madai yao

Swali: Vipi kuhusu watu wanaorefusha nywele zao?

Jibu: Kuiga katika mambo yenye manufaa ambayo hakukupokelewa kitu kutoka katika Shari´ah kinachokataza ni jambo lenye kujuzu. Ama kuiga katika mambo yenye madhara au ambayo kumepokelewa kitu kutoka katika Shari´ah chenye kukataza ndilo jambo lisilojuzu.

Watu hawa wanaorefusha nywele zao tunawaambia ya kwamba kitendo hichi kinapingana na desturi inayofuatwa katika wakati wetu huu. Kuachia nywele za kichwani ni jambo kumekhitilafiana juu yake kama ni katika Sunnah zinazotakiwa kutendewa kazi au ni katika mambo ya desturi ambayo mtu anatakiwa kufuata yale yaliyozoeleka katika wakati wake. Maoni yenye nguvu kwangu ni kwamba ni katika desturi ambazo mtu anatakiwa kufuata yale yaliyozoeleka katika wakati wake. Ikiwa ni katika desturi za watu kuachia na kurefusha nywele basi na yeye afanye hivo. Ikiwa vilevile ni katika desturi za watu kunyoa au kupunguza nywele basi na yeye afanye hivo.

Bali janga lililo kubwa kabisa ni kwamba watu hawa ambao wanafuga nywele zao za kichwani wanafanya hivo lakini wakati huo huo hawafugi ndevu zao. Kisha wakati huohuo wanadai kuwa wanamfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wao katika hayo si wakweli. Wanafuata matamanio yao na ni dalili inayothibitisha kutomfuata kwao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Utawaona kuwa ni wenye kuacha baadhi ya mambo ya wajibu kama mfano wa kufuga ndevu. Si wenye kufuga ndevu ilihali wameamrishwa kuziachia. Isitoshe wanachukulia wepesi jambo la swalah na mambo ya wajibu mengine. Ni dalili tosha yenye kuonyesha kuwa matendo yao ya kuachia nywele kichwani lengo lake sio kujikurubisha kwa Allaah wala kumfuata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Inahusiana na jambo waliloonelea kuwa ni zuri, wakalipenda na hapo wakalifuata.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (11/119)
  • Imechapishwa: 28/06/2017