Nianze na kitu gani katika kutafuta elimu?

Swali: Mimi ni kijana ambaye nimeongozwa na Allaah (´Azza wa Jall) na ni mwenye kujitahidi katika kutafuta elimu kwelikweli. Lakini sijui nianze na kitu gani katika kutafuta elimu. Hifdhi yangu imekuwa nzito pindi ninapotaka kuhifadhi na nina uelewa mchache.

Jibu: Mwanafunzi anatakiwa aanze na zile elimu ndogondogo kabla ya kubwakubwa. Kwa mfano kama anataka kujifunza elimu kuhusu ´Aqiydah basi atazame kitabu kidogo kilichoandikwa kuhusu ´Aqiydah ambapo akihifadhi na kujengea juu yake. Vivyo hivyo katika Fiqh, Hadiyth na elimu nyenginezo. Lakini kitu muhimu zaidi anachotakiwa kukitilia umuhimu ni Qur-aan. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ مُبَارَكٌ لِّيَدَّبَّرُوا آيَاتِهِ

“Kitabu Tumekiteremsha kwako hali ya kuwa ni chenye baraka ili wapate kuzingatia Aayah zake.”[1]

Kitu muhimu zaidi ambacho mtu anatakiwa kuanza nacho ni Qur-aan. Anatakiwa kukisoma, kukihifadhi, kukizingatia na kukielewa. Halafu yakufuata ni zile Sunnah zilizosihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kisha yakufuata ni maneno ya wanachuoni.

Namnasihi mwanafunzi huyu alazimiane na Shaykh maalum ambaye anamwamini elimu yake, amana yake na dini yake. Shaykh huyo atamwelekeza katika yale anayoona kuwa ni yenye manufaa zaidi kwake.

[1] 38:29

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (49) http://binothaimeen.net/content/1120
  • Imechapishwa: 22/06/2020