Ni muda kiasi gani mtu anaweza kwenda kumswalia maiti kaburini?

Swali: Imethibiti kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswali juu ya jeneza kaburini baada ya kuzikwa kwa muda. Je, inajuzu kwa mtu kumswalia ndugu yake kaburini akija kwenye kaburi lake ndani ya siku kumi tangu kufa kwake, chini ya hapo au zaidi?

Jibu: Sunnah ni kuswali juu ya kaburi ikiwa mtu hakuwa amemswalia maiti. Inapendeza amswalie kaburini. Imethibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alitajiwa kuhusu mwanamke aliyekuwa akisafisha msikiti, mwanamke mweusi aliyekuwa akisafisha msikiti. Akafa usiku ambapo waislamu wakamwosha, wakamswalia na wakamzika usiku. Kwa maana nyingine hawakumjulisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) jambo hilo, kwa sababu walichukizwa kumwamsha. Ilipofika asubuhi wakamjulisha ambapo akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Mbona hamkunijulisha? Nionyesheni kaburi lake.”

Wakamuonyesha ambapo akamswalia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akasema:

”Asife mmoja wa waislamu isipokuwa mnijulishe, kwani Allaah anafanya swalah yangu juu yao kuwa kheri kwao”  na akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): ”Ni nuru kwao.”

Hii ndiyo Sunnah. Ikiwa mtu amekosa kumswalia maiti, basi inapendekezwa akipata fursa aende akamswalie kaburini. Hii ndio Sunnah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alilifanya mara kadhaa. Pia alimswalia juu ya kaburi la Umm Sa´d na alikuwa amezikwa yapata mwezi.

Wanazuoni wametaja kuwa ikiwa ni mwezi au karibu na hapo na chini ya hapo, hakuna tatizo. Ikiwa muda umekuwa mrefu, hakuna haja ya kufanya hivyo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakufanya hivyo baada ya kupita muda mrefu. Alifanya hivyo katika mipaka ya mwezi au chini ya hapo. Lakini ikiwa muda umepita sana kwa maiti, basi haisuniwi kumswalia yule ambaye ameikosa.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1011/هل-يصلى-على-الميت-في-القبر-وما-مدة-ذلك
  • Imechapishwa: 08/01/2026