Swali: Ni lini shirki ya matamshi inakuwa kufuru kubwa?

Jibu: Anapomuomba asiyekuwa Allaah.

Swali: Akisema hali ya kuwa ni mwenye kuhalalisha jambo hilo?

Jibu: Hata kama hahalalishi. Akimuomba asiyekuwa Allaah inakuwa kufuru kubwa. Haijalishi kitu hata kama atasema kuwa hahalalishi jambo hilo.

Swali: Nakusudia katika jambo la kuapa?

Jibu: Kuapa kwa asiyekuwa Allaah ni kufuru ndogo. Isipokuwa atakapoona kuwa yule anayemuapia anajua mambo yaliyofichikana na kwamba anaendesha ulimwengu. Katika hali hiyo inakuwa kufuru kubwa kwa upande wa ´Aqiydah. Kuhusu upande wa kuapa kwa asiyekuwa Allaah kwa sababu anayemuapia anaona kuwa ni mtukufu kama vile Malaika, Mtume na mfano wao, hapo inakuwa ni shirki ndogo.

Swali: Baadhi ya washereheshaji wa vitabu wanasema kuwa shirki ya matamshi inaweza kuwa kubwa yenye kumtoa mtu nje ya dini pale ambapo mwenye kufanya hivo atahalalisha jambo hilo, akalichukulia wepesi au akalifanyia dhihaka.

Jibu: Ni kweli:

قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Sema:  Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake?”  Msitoe udhuru; mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.”[1]

Akiichezea shere dini, Mtume au Allaah inakuwa kufuru kubwa. Au yule mwenye kuapa kwa asiyekuwa Allaah anaamini kuwa anayemuapia anaendesha ulimwengu, ananufaisha na kudhuru au anajua mambo yaliyofichikana, katika hali hiyo inakuwa kufuru kubwa kwa sababu ya imani hiyo. Lakini ikimpitikia ulimini pasi na kukusudia, kama ilivyowapitia Maswahabah mwanzoni mwa Uislamu ambapo walikuwa wakiapa kwa majina ya baba zao, katika hali hiyo inakuwa ni shirki ndogo.

[1] 09:65-66

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/22062/متى-يكون-شرك-الالفاظ-كفرا-اكبر
  • Imechapishwa: 25/10/2022