Ni ipi hukumu ya kuzidisha matamshi kwenye adhaana?

Swali: Ni ipi hukumu ya kuzidisha katika adhaana?

Jibu: Adhaana ni ´ibaadah iliyosuniwa kwa matamshi maalum ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewabainishia ummah wake kwa kuyapitisha. Kwa hivyo haijuzu kwa mtu kuvuka mipaka ya Allaah (Ta´ala) au akazidisha kitu kutoka kwake ambacho hakikuthibiti kwa dalili. Mwenye kufanya hivo, basi anarudishiwa mwenyewe. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayezua katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo basi atarudishiwa mwenyewe.”[1]

Imekuja katika tamko jengine:

“Yeyote atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu basi atarudishiwa mwenyewe.”[2]

Mtu akizisha kitu kwenye adhaana ambacho hakikuthibiti kwa andiko anakuwa ametoka nje yale aliyokuwemo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na waislamu katika yale aliyozidisha. Waislamu wote wanatambua kuwa Shari´ah inachukuliwa kutoka kwa Mwekaji Shari´ah. Kwa hivyo tunapaswa kumwabudu Allaah kwa yale ambayo Shari´ah imekuja nayo, ima iwe kwa njia ya mapendezo au wajibu. Ikiwa Shari´ah haikuja na jambo, basi hatuna haki ya kumtangulia mbele Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kuzidisha au kupunguza kitu.

[1] Muslim (1718).

[2] al-Bukhaariy (2697).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/197-198)
  • Imechapishwa: 10/08/2026