Ni ipi hukumu ya kuwaomba wahudhuriaji wamshuhudilie maiti?

Swali: Baadhi ya waislamu wanawaomba maiti kutamka shahaadah kabla ya kuzikwa. Kwa mfano ndugu au mlezi wa maiti anawauliza wahudhuriaji wanachomshuhudilia yule maiti ambapo wanamshuhudilia wema na kuwa na msimamo. Je, hili lina asli katika Shari´ah?

Jibu: Halina asli katika Shari´ah. Haifai kuwataka watu wamshuhudilie maiti. Ni katika Bid´ah. Wanaweza kumshuhudilia shari na ikaja kuwa ni fedheha kwake. Kilichothibiti katika Sunnah ni kuwa jeneza lilipitishwa mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa pamoja na Maswahabah wake (Radhiya Allaahu ´anhum) ambapo wakamsifu yule maiti. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Imewajibika.” Kisha kukapita jeneza lingine ambalo wakalisema vibaya. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Imewajibika.” Alipoulizwa ni kwa nini amesema: “Imewajibika” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Yule mliyemsifu ataingia Peponi ikawa ni wajibu kwake kuingia Peponi na huyu mmesema vibaya ikawa ni wajibu kwake kuingia Motoni. Nyinyi ni mashahidi wa Allaah juu ya ardhi. Nyinyi ni mashahidi wa Allaah juu ya ardhi. Nyinyi ni mashahidi wa Allaah juu ya ardhi.”[1]

[1] al-Bukhaariy (1367) na Muslim (949).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/217)
  • Imechapishwa: 07/08/2021