Ni ipi hukumu ya kutembelea kaburi la mama yake Mtume

Muheshimiwa Shaykh na baba Muhammad bin Swaalih al-´Uthaymiyn – Allaah akuwafikishe.

السلام عليكم ورحمة الله وبركاته

Baadhi ya ndugu wanaenda al-Abwaa´ na wanadai kuwa ndio mahali lilipo kaburi la mama yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanafanya Tawassul kwaye na baadhi yao wanamwomba moja kwa moja awaondoshee matatizo na huduma nyinginezo. Pengine matendo yao yanatokana na kwamba wanaamini kuwa Allaah alimuhuisha kisha akamwamini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kisha akafariki. Ni ipi hukumu ya kulitembelea kaburi lake ikisihi kweli kuzikwa mahali hapo? Je, ni sahihi kwamba alihuishwa na kumwamini? Ni ipi hukumu ya kumwomba mtu ambaye kishakufa na kumwomba akuondoshee matatizo? Je, inafaa kwa mtu kuwaomba Mitume ambao wameshakufa na waja wengine wema?

Jibu:

بسم الله الرحمن الرحيم

و عليكم السلام و رحمة الله و بركاته

Mahali ambapo inasemekana kuwa lipo kaburi la mama yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakujulikani katika kipindi cha hapo kabla. Mambo yakishakuwa hivo basi madai ya wale waliokuja nyuma yatakuwa hayana dalili. Kwa hivo kule kulenganisha si venginevyo isipokuwa ni kufuata dhana tu ambayo haitoshelezi kutokaamana na haki chochote. Kwa ajili hiyo wale wanaotembelea kaburi hilo wanakuwa ni wenye kukosea kwa njia zifuatazo:

1 – Haikuthibiti kwamba kaburi lake liko maeneo hapo. Kwa hivyo wanakuwa ni wenye kufuata yale ambayo hawana elimu nayo.

2 – Kulitembelea si jambo lenye kupendeza. Kwa ajili hiyo Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) hawakulitembelea, ilihali wao wanampenda Mtume (Swaall Allaahu ´alayhi wa sallam) zaidi kutushinda na wenye kuzifuata Sunnah zake zaidi kutushinda. Mtume (Swaall Allaahu ´alayhi wa sallam) alilitembelea kaburi la mama yake kwa njia ya huruma ya mtoto kwa mama yake. Hata hivyo hakumuombea msamaha. Muslim amepokea kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba Mtume wa Allaah (Swaall Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nilimuomba idhini Mola wangu kumuombea msamaha mamangu, hakunipa ruhusa. Nikamuomba idhini ya kutembelea kaburi lake, akanipa ruhusa.”[1]

3 – Kufanya Tawassul naye ni miongoni mwa zile Tawassul zilizokatazwa. Ni shirki kufanya Tawassul na waislamu waliokufa. Tusemeje kufanya Tawassul kwa mtu ambaye amekufa kabla ya Ujumbe na ambaye Mtume (Swaall Allaahu ´alayhi wa sallam) amekatazwa kumuombea msamaha?

4 – Ni shirki kubwa kuwaomba wafu wakuondoshee matatizo. Kitendo kama hicho kinamtoa mwenye nacho nje ya Uislamu na ni upumbavu na upotofu. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَنْ أَضَلُّ مِمَّن يَدْعُو مِن دُونِ اللَّـهِ مَن لَّا يَسْتَجِيبُ لَهُ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ وَهُمْ عَن دُعَائِهِمْ غَافِلُونَ وَإِذَا حُشِرَ النَّاسُ كَانُوا لَهُمْ أَعْدَاءً وَكَانُوا بِعِبَادَتِهِمْ كَافِرِينَ

”Ni nani aliyepotea zaidi kuliko yule anayemwomba badala ya Allaah, ambao hatowaitikia mpaka siku ya Qiyaamah nao hawatambui maombi yao. Na [Qiyaamah] watakapokusanywa watu [miungu ya uongo] watakuwa maadui wao na watakuwa kwa ‘ibaadah zao ni wenye kuzikanusha.”[2]

وَمَن يَرْغَبُ عَن مِّلَّةِ إِبْرَاهِيمَ إِلَّا مَن سَفِهَ نَفْسَهُ

“Na nani atakayejitenga na imani ya Ibraahiym isipokuwa anayeitia nafsi yake upumbavu?”[3]

Kuhusu kuamini kuwa Allaah (Ta´ala) alimuhuisha mama yake na Mtume (Swaall Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akamwamini kisha baadaye akafariki, hakika imani kama hii ni batili na haina msingi wowote. Hadiyth iliyopokelewa juu yake imetungwa.

Kitendo cha mtu kuwa Mtume au mja mwema hakijuzishi watu kumuomba. Mtume na waja wema hawaridhii kitendo hicho.

Muhammad bin Swaalih al-´Uthaymiyn

1419-02-14

[1] Muslim (976).

[2] 46:5-6

[3] 2:130

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/309-311)
  • Imechapishwa: 26/09/2022