06. Ni ipi hukumu ya kutamba kwa hanchifu?

Swali 06: Ni ipi hukumu ya kutamba kwa hanchifu? Je, jiwe moja linatosha wakati wa kutamba[1]?

Jibu: Inafaa kutamba kwa kila kitu katika vitu visafi ambavyo vinaondosha uchafu; kama mfano wa kokoto, matofali yaliyotengenezwa kwa udongo, tishu safi, karatasi safi ambazo hazina kitu katika utajo wa Allaah au majina Yake au vyenginevyo ambavyo vinafanywa kufikiwa yale malengo. Katika vitu hivyo kunavuliwa mifupa na kinyesi. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kutamba kwavyo na akasema:

“Havisafishi.”

Katika “as-Swahiyh” ya Muslim amepokea kupitia kwa Salmaan al-Faarisiy (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametukataza kuelekea Qiblah wakati wa kukidhi haja kubwa au ndogo, kutamba kwa mkono wa kuume, kutamba chini ya mawe matatu au kutamba kwa kinyesi au mfupa.”[2]

Muslim amepokea tena katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kutamba kwa mfupa au kinyesi” na akasema: “Ni chakula cha ndugu zenu katika majini.”[3]

Haisihi kutamba kwa mawe chini ya matatu kutokana na Hadiyth ya Salmaan iliyotajwa na nyenginezo zilizopokelewa katika mada hiyo. Kusiposafika basi yule mwenye kujitamba atalazimika kuzidisha jiwe la nne au zaidi ya hivo mpaka pasafike pale pahali.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (10/37).

[2] Muslim (605).

[3] Muslim (606).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Musaafir, uk. 17-18
  • Imechapishwa: 21/02/2022